Popular Posts

Recent Posts

OKWI KUREJEA MSIMBAZI

06:33 Add Comment

UONGOZI wa Simba umesema unafanya mpango wa kumrejesha kikosini mshambuliaji wake wa zamani Emmanuel Okwi aliyevunja mkataba na klabu ya Sonderjyske ya Denmark.
Taarifa za kwenye mtandao wa klabu hiyo juzi ziliandika kwamba Okwi amefikia makubaliano ya kuvunja mkataba baada ya kukosa nafasi ya kucheza kwenye kikosi hicho.
Jana jioni Ofisa habari wa Simba, Haji Manara aliandika kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii: “Kocha Omog (Joseph- kocha mkuu wa Simba) ikimpendeza, Emmanuel Okwinho (Okwi) dimbani Feb 18, hiyo ndio habari mpasuko, ukinuna ongeza limao,”.
Simba inatarajia kucheza na Yanga katika mechi ya raundi ya pili ya Ligi Kuu baada ya kutoka sare ya bao 1-1 katika mechi ya kwanza.
Alipoulizwa na gazeti hili kuhusu taarifa hizo, Manara alikiri kuwa uongozi wake uko kwenye mchakato wa kumnasa mchezaji huyo na ikiwezekana atumike kwenye mechi zilizosalia za Ligi Kuu.
“Ni kweli tutamsajili kama mchezaji huru,” alisema.
Hata hivyo, tayari dirisha dogo la usajili kwa klabu za ligi limeshafungwa mpaka msimu ujao. Akilizungumzia hilo, ofisa habari wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas alisema Simba haiwezi kumtumia Okwi kwa sababu dirisha la usajili limeshafungwa.
“Ingewezekana kama usajili wa dirisha dogo ungekuwa haujafungwa, lakini dirisha limeshafungwa hivyo kama wanataka kumtumia, wasubiri mpaka usajili mwingine,” alisema.
Wakati wa usajili wa dirisha dogo Desemba mwaka jana Simba ilitaka kumsajili mshambuliaji huyo Mganda lakini ilishindwa baada ya klabu ya Sonderjyske kutaka ilipwe karibu sh milioni 240.
Hasimu wa Simba, Yanga pia ilijaribu kutaka kusajili mshambuliaji mwingine ili ashindane na Donald Ngoma baada ya kudaiwa kugoma kucheza kwenye mechi za kombe la Mapinduzi lakini ilishindikana kwa vile dirisha la usajili lilishafungwa.
Sonderjyske ilimsajili Okwi Julai 2015 kutoka Simba kwa mkataba wa miaka mitano uliotakiwa kumalizika mwaka 2020 ambapo tangu amesajiliwa Okwi alicheza mechi nne tu za Ligi Kuu ya Denmark na mbili za kombe la DBU ambapo alifunga mabao mawili.
Simba pia iliwahi kumuuza Okwi Etoile du Sahel ya Tunisia mwaka 2013 kwa dola za Marekani 300,000 kabla ya kusajiliwa na Yanga alipocheza kwa muda mfupi na kurejea Simba.
Okwi ni mshambuliaji kipenzi cha wanasimba kutokana na mafanikio aliyoipatia timu hiyo ambapo jana baada ya Manara kuweka suala lake kwenye mitandao ya kijamii, karibu mashabiki wengi wa soka walikuwa wakimzungumzia.

MATOKEO YA LEO YATAAMUA

06:45 Add Comment

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu bara, Yanga jana iliifunga Majimaji ya mjini hapa bao 1-0 katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja wa Majimaji na kujiongezea pointi tatu muhimu.
Matokeo hayo yanaifanya Yanga kufikisha pointi 43 pointi moja nyuma ya vinara Simba wenye pointi 44 ambao wanacheza leo na Mtibwa Sugar.
Aidha matokeo hayo pia yanaiweka pabaya Simba kwani sasa italazimika kushinda mechi yake ya leo kama inataka kuendelea kuongoza kwa tofauti ya pointi nne.
Yanga ilianza kulisakama lango la Majimaji mapema mwanzoni mwa mchezo huo ambapo katika dakika ya saba Simon Msuva nusura aandike bao lakini akiwa peke yake na kipa shuti lake lilipaa juu ya lango la Majimaji.
Bao la Yanga lilifungwa katika dakika ya 13 na Deus Kaseke aliyetumia vema makosa yaliyofanywa na kipa wa Majimaji, Aghton Antony aliyetema shuti la Msuva kabla mfungaji hajaliwahi na kuujaza mpira wavuni.
Kuingia kwa bao hilo kulizidisha ari kwa wachezaji wa Yanga ambao mwanzo walionekana kama kucheza kwa tahadhari na hivyo kuwabana zaidi wapinzani wao ambao nao walionekana kuwa na uwezo wa kurudisha bao hilo kutokana na mchezo waliokuwa wakicheza.
Hata hivyo, pamoja na jitihada za Majimaji hazikuzaa matunda na matokeo yake walikwenda mapumziko wakiwa nyuma ya bao 1-0 dhidi ya wageni wao.
Yanga ilianza tena mechi hiyo kwa kasi na dakika ya 48 Msuva tena akiwa kwenye nafasi nzuri ya kufunga, alipiga mpira nje.
Aidha mechi hiyo ilikuwa na rabsha za hapa na pale ambapo wachezaji wa Yanga kabla ya mechi kuanza na waligoma kuingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo wakidai kufanyiwa mambo ya kishirikina, kitendo ambacho walikifanya tena wakati wa mapumziko ambapo walibaki uwanjani wakigoma kuingia vyumbani.
Matokeo hayo yamezidi kuiweka pabaya Majimaji inayopambana kutoshuka daraja kwani imebaki katika nafasi yake ya 14 kwenye msimamo ikiwa na pointi 17.
Timu zilikuwa:

Yanga: Deogratius Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Haji Mwinyi, Andrew Vincent, Kelvin Yondani, Thaban Kamusoko, Simon Msuva, Haruna Niyonzima/Oscar Joshua, Amissi Tambwe, Juma Mahadhi na Deus Kaseke/Said Juma ‘Makapu.

Maji Maji: Agathon Anthony, Salehe Mohammed, Mpoki Mwakinyuke, Keneddy Kipepe, Bahati Yussuf/Emmanuel Semwanza, Yakoub Kibiga/Paul Nyangwe, Iddi kipwagile, Kelvin Kongwa, George Mpole, Hassan Hamisi na Lucas Kikoti/Peter Mapunda.

UGANDA YAPATA KIPIGO

06:36 Add Comment

Andre Ayew alifunga bao la pekee la mechi dhidi ya Uganda katika mechi ya ufunguzi ya kundi D katika michuano ya kombe la bara Afrika linaloendelea nchini Gabon.
Winga huyo wa klabu ya West Ham alifunga bao la penalti kunako dakika ya 32 baada ya nahodha Asamoah Gyan kuvutwa katika eneo la hatari.
Ghana pia ilitishia kupitia vichwa viwili vya Gyan ,huku Ayew na Christian Atsu wakimjaribu kipa wa Uganda Denis Onyango.
Uganda walikaribia lango la Ghana baada ya Faruku Miya kupiga mwamba wa goli lakini hawakuweza kusawazisha.
Uganda wanaocheza kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1978 hawakuwa na bahati.
Cranes walitengeza fursa chache na walishindwa kuingia katika lango la Ghana ambao walifurahia kulinda lango lao .

ALIYEMTABIRIA KIFO MUGABE AKAMATWA

06:34 Add Comment

Maafisa wa polisi nchini Zimbabwe wamemkamata na kumzuilia mhubiri aliyetabiri kwamba Rais Robert Mugabe atafariki mwezi Oktoba mwaka huu.
Pasta Patrick Mugadza alikamatwa akiwa mahakamani mjini Harare Jumatatu ambapo alikuwa ameenda kwa kesi nyingine dhidi yake, wakili wake Gift Mtisi ameambia wanahabari.
Alikuwa anakabiliwa na mashtaka ya kuvalia bendera ya taifa
"Alikuwa amefika mahakamani kwa kesi hiyo polisi walipomkamata wakati wa mapumziko na kumfungulia mashtaka kwa sababu ya unabii huo," Bw Mtisi aliambia AFP.
"Awali alishtakiwa kwa kudunisha na kukosea heshima mamlaka ya rais lakini shtaka hilo likabadilishwa baadaye na kuwa kuwatusi watu wa asili fulani au dini fulani."
Pasta Mugadza, ambaye huhudumu katika mji wa Kariba kaskazini mwa nchi hiyo, aliandaa kikao na wanahabari wiki iliyopita ambapo alitabiri kwamba Mugabe angefariki Oktoba 17 mwaka huu.

Kumfanyia mzaha Rais Mugabe au kutoa unabii au ubashiri kumhusu ni jambo hatari nchini Zimbabwe.
Nchini humo kuna sheria ambayo huharamisha "kudunisha mamlaka ya au kumtusi rais."
Mwaka 2015, Mugadza alikamatwa na kuzuiliwa kwa karibu mwezi mmoja baada ya kujitokeza hadharani na bango lililokuiwa na ujumbe uliomwambia Mugabe kwamba watu wamekuwa wakiteseka chini ya utawala wake.
Siku ya maadhimisho ya uhuru mwaka jana, alitoa mahubiri akiwa amejifungia kwenye boriti ya taa nje ya duka kubwa zaidi la kibiashara mjini Harare, akisema hiyo ilikuwa ishara ya raia kukandamizwa Zimbabwe.
Rais Mugabe amekuwa madarakani tangu 1980.
Kumekuwa na uvumi kuhusu afya yake na mara kwa mara husafiri mataifa ya Asia kwa matibabu.

Bw Mugabe amekataa kumtaja mrithi wake na chama chake cha ZANU-PF kimekuwa kikiyumbishwa na makundi ya watu wanaotaka kumrithi.
Mwishoni mwa mwaka uliopita, raia na wafuasi wa vyama vya upinzani waliandamana kupinga utawala wake.

WAZIRI APIGWA KOFI UFARANSA

06:30 Add Comment

Waziri mkuu mstaafu wa Ufaransa Manuel Valls amekashifiwa alipokuwa akihamasisha katika kampeni za chama cha kisoshalisti katika uchaguzi mkuu wa kiti cha Urais nchini Ufaransa.
Alipokuwa akihutubia katika ukanda wa Magharibi mwa mji wa Brittany alipigwa kofi na kijana mdogo alipokuwa akisalimia kwa kushikana mikono.
Mlinzi binafsi wa Bwana Valls alimkamata kijana huyo kooni kisha akamtupa chini.
Manuel Valls hajajeruhiwa katika tukio hili.

WAFUNGWA 30 WAFARIKI KATIKA MACHAFUKO BRAZIL

06:14 Add Comment

Taarifa za kutisha zimeanza kujitokeza nchini Brazil kutokana na machafuko yaliyotokea usiku kucha katika jela la Alcaçuz baada ya kuibuka kwa mgomo.
Mamlaka nchini Brazil zinasema takriban wafungwa thelathini waliuawa na wafungwa wenzao, wataalamu wakuchunguza masuala ya mauwaji wamesema walioathirika zaidi walikuwa wamekatwakatwa au kutolewa baadhi ya viongo.
Mgomo huo ulianza jumamosi mchana, wanakikundi wa kikundi cha wahalifu waliopo katika magereza ya Brazil na kushambulia kundi hasimu lenye msimamo tofauti.
Hii ni mara ya tatu kwa mgomo mkubwa kama huu kujitokeza kwa wafungwa nchini Brazil mwezi huu, mamia ya wafungwa wamefariki gerezani katika miji ya Amazonas na Roraima.

MAHAKAMA YAIAMURU KAMPUNI YA KENYA KULIPA FIDIA

07:06 Add Comment

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara imeiamuru kampuni ya Uingereza yenye makao yake Kenya, British American Tobacco Kenya Limited (BAT), kuilipa fidia ya Sh6.2 bilioni kampuni ya Mohan’s Oysterbay Drinks Limited ya nchini.
Uamuzi huo unatokana na Mahakama kuridhika kuwa kulikuwa na makubaliano ya kibiashara kati ya Mohan’s na BAT ambayo iliyavunja.
Mohan’s iliomba kulipwa Sh12 bilioni zikiwa ni fidia ya uwekezaji iliofanya kutokana na makubaliano hayo, hasara ya kibiashara, faida waliyoitarajia, hasara ya jumla na riba. Makubaliano hayo yalihusu usambazaji wa sigara zinazozalishwa na BAT aina ya Dunhill na Benson & Hedges.
BAT ilikana kuwa na uhusiano wa kibiashara na Mohan’s kama msambazaji wa bidhaa zake kwa madai kuwa hapakuwa na mkataba wa maandishi, bali uhusianao wao ulikuwa ni muuzaji na mnunuzi.
Jaji Latifa Mansoor katika hukumu ya kesi hiyo, amesema vielelezo vilivyowasilishwa na Mohan’s mahakamani vinabainisha kulikuwa na makubaliano ya kibiashara ya mtengenezaji na msambazaji na si muuzaji na mnunuzi.
Amesema BAT haikuwa na sababu ya msingi kuvunja makubaliano kwa kuwa haikuonyesha kuwa Mohan’s ilitenda kosa la ukiukaji wa makubaliano lililosababisha kuyasitisha baada ya kuwapo uhusiano wa kibiashara wa miaka 19.
Jaji Mansoor amesema BAT ingeweza kujadiliana na Mohan’s kuhusu masharti yenye manufaa kwa makubaliano ya usambaji bidhaa hizo, huku wakiweka kifungu cha kuyasitisha jambo ambalo lingewezesha kuendeleza biashara kwa muda mrefu.
Licha ya kukubaliana na madai ya Mohan’s kuhusu uhusiano wake na BAT, hata hivyo Jaji Mansoor hakukubaliana na kiwango cha fidia ambacho kampuni hiyo ya Mohan’s ilikuwa imekiomba cha Sh12,079,000,000.
Badala yake Jaji Mansoor ameamuru kampuni hiyo ya BAT kuilipa Mohan’s fidia ya jumla ya Sh6,234,835,855 (zaidi ya Sh6.2 bilioni), ikiwa ni fidia ya hasara ya gharama za uwekezaji, hasara ya kibiashara, hasara ya jumla,
Pia ameiamuru BAT kulipa asilimia 12 ya kiasi hicho tangu siku ya hukumu hadi itakapokamilisha malipo hayo na pia kulipa gharama zote za kesi hiyo.
Jaji amesema katika hukumu hiyo kuwa kampuni hiyo imeshindwa kuthibitisha madai mengine kiasi cha Sh12 bilioni ilichokuwa ikiomba, kama vile mapato ya mauzo waliyokuwa wakiyatarajia, malipo ya fidia na malipo ya bima kwa wafanyakazi waliowapunguza.
Mohan’s kupitia kwa Wakili wake Dillip Kesaria ililieleza Mwananchi kuwa ingawa madai yake ya fidia ya zaidi ya Sh12 bilioni iliyokuwa ikiiomba hayakukubaliwa, lakini wameridhika na hukumu hiyo na kiasi cha zaidi ya Sh6.2 bilioni walizopewa na Mahakama.
Wakati Mohan’s ikieelezea kuridhika na hukumu hiyo, BAT kwa upande wake kupitia kwa Wakili wake, Karume, ililieleza kuwa haikuridhika na hukumu hiyo na kwamba itakata rufaa katika Mahakama ya Rufani kuipinga.
Wakili Karume alibainisha kuwa tayari wameshachukua hatua za awali za kukata rufaa kuipinga hukumu hiyo, kwa kuwasilisha mahakamani taarifa ya kusudio la kukata rufaa.
“Hivyo kwa sasa tunasubiri tu kupata mwenendo wa kesi hiyo ili tuweze kukata rufaa rasmi kwa kuwasilisha mahakamani sababu za rufaa yetu,”amesema Wakili Karume.

Total Pageviews