MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu bara, Yanga jana iliifunga Majimaji ya mjini hapa bao 1-0 katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja wa Majimaji na kujiongezea pointi tatu muhimu.
Matokeo hayo yanaifanya Yanga kufikisha pointi 43 pointi moja nyuma ya vinara Simba wenye pointi 44 ambao wanacheza leo na Mtibwa Sugar.
Aidha matokeo hayo pia yanaiweka pabaya Simba kwani sasa italazimika kushinda mechi yake ya leo kama inataka kuendelea kuongoza kwa tofauti ya pointi nne.
Yanga ilianza kulisakama lango la Majimaji mapema mwanzoni mwa mchezo huo ambapo katika dakika ya saba Simon Msuva nusura aandike bao lakini akiwa peke yake na kipa shuti lake lilipaa juu ya lango la Majimaji.
Bao la Yanga lilifungwa katika dakika ya 13 na Deus Kaseke aliyetumia vema makosa yaliyofanywa na kipa wa Majimaji, Aghton Antony aliyetema shuti la Msuva kabla mfungaji hajaliwahi na kuujaza mpira wavuni.
Kuingia kwa bao hilo kulizidisha ari kwa wachezaji wa Yanga ambao mwanzo walionekana kama kucheza kwa tahadhari na hivyo kuwabana zaidi wapinzani wao ambao nao walionekana kuwa na uwezo wa kurudisha bao hilo kutokana na mchezo waliokuwa wakicheza.
Hata hivyo, pamoja na jitihada za Majimaji hazikuzaa matunda na matokeo yake walikwenda mapumziko wakiwa nyuma ya bao 1-0 dhidi ya wageni wao.
Yanga ilianza tena mechi hiyo kwa kasi na dakika ya 48 Msuva tena akiwa kwenye nafasi nzuri ya kufunga, alipiga mpira nje.
Aidha mechi hiyo ilikuwa na rabsha za hapa na pale ambapo wachezaji wa Yanga kabla ya mechi kuanza na waligoma kuingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo wakidai kufanyiwa mambo ya kishirikina, kitendo ambacho walikifanya tena wakati wa mapumziko ambapo walibaki uwanjani wakigoma kuingia vyumbani.
Matokeo hayo yamezidi kuiweka pabaya Majimaji inayopambana kutoshuka daraja kwani imebaki katika nafasi yake ya 14 kwenye msimamo ikiwa na pointi 17.
Timu zilikuwa:
Yanga: Deogratius Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Haji Mwinyi, Andrew Vincent, Kelvin Yondani, Thaban Kamusoko, Simon Msuva, Haruna Niyonzima/Oscar Joshua, Amissi Tambwe, Juma Mahadhi na Deus Kaseke/Said Juma ‘Makapu.
Maji Maji: Agathon Anthony, Salehe Mohammed, Mpoki Mwakinyuke, Keneddy Kipepe, Bahati Yussuf/Emmanuel Semwanza, Yakoub Kibiga/Paul Nyangwe, Iddi kipwagile, Kelvin Kongwa, George Mpole, Hassan Hamisi na Lucas Kikoti/Peter Mapunda.
EmoticonEmoticon