Showing posts with label KITAIFA. Show all posts
Showing posts with label KITAIFA. Show all posts

ALIYEMTABIRIA KIFO MUGABE AKAMATWA

06:34 Add Comment

Maafisa wa polisi nchini Zimbabwe wamemkamata na kumzuilia mhubiri aliyetabiri kwamba Rais Robert Mugabe atafariki mwezi Oktoba mwaka huu.
Pasta Patrick Mugadza alikamatwa akiwa mahakamani mjini Harare Jumatatu ambapo alikuwa ameenda kwa kesi nyingine dhidi yake, wakili wake Gift Mtisi ameambia wanahabari.
Alikuwa anakabiliwa na mashtaka ya kuvalia bendera ya taifa
"Alikuwa amefika mahakamani kwa kesi hiyo polisi walipomkamata wakati wa mapumziko na kumfungulia mashtaka kwa sababu ya unabii huo," Bw Mtisi aliambia AFP.
"Awali alishtakiwa kwa kudunisha na kukosea heshima mamlaka ya rais lakini shtaka hilo likabadilishwa baadaye na kuwa kuwatusi watu wa asili fulani au dini fulani."
Pasta Mugadza, ambaye huhudumu katika mji wa Kariba kaskazini mwa nchi hiyo, aliandaa kikao na wanahabari wiki iliyopita ambapo alitabiri kwamba Mugabe angefariki Oktoba 17 mwaka huu.

Kumfanyia mzaha Rais Mugabe au kutoa unabii au ubashiri kumhusu ni jambo hatari nchini Zimbabwe.
Nchini humo kuna sheria ambayo huharamisha "kudunisha mamlaka ya au kumtusi rais."
Mwaka 2015, Mugadza alikamatwa na kuzuiliwa kwa karibu mwezi mmoja baada ya kujitokeza hadharani na bango lililokuiwa na ujumbe uliomwambia Mugabe kwamba watu wamekuwa wakiteseka chini ya utawala wake.
Siku ya maadhimisho ya uhuru mwaka jana, alitoa mahubiri akiwa amejifungia kwenye boriti ya taa nje ya duka kubwa zaidi la kibiashara mjini Harare, akisema hiyo ilikuwa ishara ya raia kukandamizwa Zimbabwe.
Rais Mugabe amekuwa madarakani tangu 1980.
Kumekuwa na uvumi kuhusu afya yake na mara kwa mara husafiri mataifa ya Asia kwa matibabu.

Bw Mugabe amekataa kumtaja mrithi wake na chama chake cha ZANU-PF kimekuwa kikiyumbishwa na makundi ya watu wanaotaka kumrithi.
Mwishoni mwa mwaka uliopita, raia na wafuasi wa vyama vya upinzani waliandamana kupinga utawala wake.

MAHAKAMA YAIAMURU KAMPUNI YA KENYA KULIPA FIDIA

07:06 Add Comment

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara imeiamuru kampuni ya Uingereza yenye makao yake Kenya, British American Tobacco Kenya Limited (BAT), kuilipa fidia ya Sh6.2 bilioni kampuni ya Mohan’s Oysterbay Drinks Limited ya nchini.
Uamuzi huo unatokana na Mahakama kuridhika kuwa kulikuwa na makubaliano ya kibiashara kati ya Mohan’s na BAT ambayo iliyavunja.
Mohan’s iliomba kulipwa Sh12 bilioni zikiwa ni fidia ya uwekezaji iliofanya kutokana na makubaliano hayo, hasara ya kibiashara, faida waliyoitarajia, hasara ya jumla na riba. Makubaliano hayo yalihusu usambazaji wa sigara zinazozalishwa na BAT aina ya Dunhill na Benson & Hedges.
BAT ilikana kuwa na uhusiano wa kibiashara na Mohan’s kama msambazaji wa bidhaa zake kwa madai kuwa hapakuwa na mkataba wa maandishi, bali uhusianao wao ulikuwa ni muuzaji na mnunuzi.
Jaji Latifa Mansoor katika hukumu ya kesi hiyo, amesema vielelezo vilivyowasilishwa na Mohan’s mahakamani vinabainisha kulikuwa na makubaliano ya kibiashara ya mtengenezaji na msambazaji na si muuzaji na mnunuzi.
Amesema BAT haikuwa na sababu ya msingi kuvunja makubaliano kwa kuwa haikuonyesha kuwa Mohan’s ilitenda kosa la ukiukaji wa makubaliano lililosababisha kuyasitisha baada ya kuwapo uhusiano wa kibiashara wa miaka 19.
Jaji Mansoor amesema BAT ingeweza kujadiliana na Mohan’s kuhusu masharti yenye manufaa kwa makubaliano ya usambaji bidhaa hizo, huku wakiweka kifungu cha kuyasitisha jambo ambalo lingewezesha kuendeleza biashara kwa muda mrefu.
Licha ya kukubaliana na madai ya Mohan’s kuhusu uhusiano wake na BAT, hata hivyo Jaji Mansoor hakukubaliana na kiwango cha fidia ambacho kampuni hiyo ya Mohan’s ilikuwa imekiomba cha Sh12,079,000,000.
Badala yake Jaji Mansoor ameamuru kampuni hiyo ya BAT kuilipa Mohan’s fidia ya jumla ya Sh6,234,835,855 (zaidi ya Sh6.2 bilioni), ikiwa ni fidia ya hasara ya gharama za uwekezaji, hasara ya kibiashara, hasara ya jumla,
Pia ameiamuru BAT kulipa asilimia 12 ya kiasi hicho tangu siku ya hukumu hadi itakapokamilisha malipo hayo na pia kulipa gharama zote za kesi hiyo.
Jaji amesema katika hukumu hiyo kuwa kampuni hiyo imeshindwa kuthibitisha madai mengine kiasi cha Sh12 bilioni ilichokuwa ikiomba, kama vile mapato ya mauzo waliyokuwa wakiyatarajia, malipo ya fidia na malipo ya bima kwa wafanyakazi waliowapunguza.
Mohan’s kupitia kwa Wakili wake Dillip Kesaria ililieleza Mwananchi kuwa ingawa madai yake ya fidia ya zaidi ya Sh12 bilioni iliyokuwa ikiiomba hayakukubaliwa, lakini wameridhika na hukumu hiyo na kiasi cha zaidi ya Sh6.2 bilioni walizopewa na Mahakama.
Wakati Mohan’s ikieelezea kuridhika na hukumu hiyo, BAT kwa upande wake kupitia kwa Wakili wake, Karume, ililieleza kuwa haikuridhika na hukumu hiyo na kwamba itakata rufaa katika Mahakama ya Rufani kuipinga.
Wakili Karume alibainisha kuwa tayari wameshachukua hatua za awali za kukata rufaa kuipinga hukumu hiyo, kwa kuwasilisha mahakamani taarifa ya kusudio la kukata rufaa.
“Hivyo kwa sasa tunasubiri tu kupata mwenendo wa kesi hiyo ili tuweze kukata rufaa rasmi kwa kuwasilisha mahakamani sababu za rufaa yetu,”amesema Wakili Karume.

DK. SHEIN KUONGOZA KIKAO CCM ZANZIBAR

06:14 Add Comment

MAKAMU Mwenyekiti wa CCM, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein, leo anatarajia kukiongoza Kikao cha Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa mjini hapa.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Katibu wa Kamati Maalumu ya NEC Zanzibar - Idara ya Itikadi na Uenezi, Waride Bakar Jabu, kikao hicho cha kawaida cha siku moja kitafanyika Ofisi Kuu ya CCM, Kisiwandui kuanzia saa 4 asubuhi.
Alisema kikao pamoja na mambo mengine, kitapokea na kujadili Mapendekezo ya wanachama wa CCM wanaoomba kuteuliwa kugombea nafasi ya Ubunge katika Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Dimani na kuongeza kuwa maandalizi yote yamekamilika.
Aidha, Katibu Waride alisema kikao hicho kilitanguliwa na Kikao cha Sekretarieti ya Kamati Maalum ya NEC, chini ya Mwenyekiti wake Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, kwa lengo la kuandaa ajenda za kikao hicho.
Wanachama wa CCM watatu wamepitishwa kuingia katika tatu bora katika kikao cha halmashauri ya jimbo la Dimani ambao ni Juma Ali Juma, Hussein Migoda pamoja na Abdalla Sheria ambao wataajaza nafasi ya mbunge wa jimbo hilo Hafidh Ali Tahir, aliyefariki dunia b aada ya kuugua ghafla usiku wa kuamkia Desemba 11 akiwa katika vikao vya Bunge mjini Dodoma.

NDEGE MPYA KUWASILI TANZANIA

23:27 Add Comment

Rais wa Tanzania John Magufuli ametangaza kwamba taifa hilo litanunua ndege zaidi katika juhudi za kufufua shirika la ndege la taifa hilo.
Amesema serikali yake imedhamiria kununua ndege nne zikiwemo ndege kubwa tatu ambazo zitasaidia kuinua "uchumi wa nchi kwa kuwezesha watalii kuja hapa nchini moja kwa moja kutoka nchi zao."
Dkt Magufuli alisema hayo baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Masoko ya Afrika wa Kampuni ya utengenezaji wa ndege ya Boeing yenye makao yake nchini Marekani Bw. Jim Deboo katika ikulu jijini Dar es Salaam.
Amesema Tanzania inpanga kununua ndege aina ya Boeing 787 Dash 8 Dreamliner yenye uwezo wa kuchukua abiria 262 ambayo inatarajiwa kuwasili nchini humo Juni 2018.
Ndege nyingine ambazo Tanzania itazinunua ni ndege moja aina Bombardier Q400 Dash 8 NextGen inayotarajiwa kuwasili Mwezi Juni 2017, ndege 2 aina ya Bombardier CS300 zenye uwezo wa kuchukua kati ya abiria 137 na 150 na zinazotarajiwa kuwasili nchini kati ya Mei na Juni, 2018.
Malipo ya awali kwa ndege hizi yameshafanyika.
"Tumeleta ndege aina ya Bombardier hapa, zimepunguza gharama za safari mfano kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza, sasa wanalipa kati ya 160,000/ hadi 200,000/- wakati nauli ilishafika Shilingi laki 8 na kitu, lakini watu wengine utakuta wanazungumzazungumza wee maneno ya hovyo kwa kutumiwa, tumeshaamua na tutafanya hivyo" amesema Rais Magufuli.
"Sisi hapa tunazungumza kuwa watalii hawajafika hata milioni 2 kwa mwaka, lakini nchi kama Morocco inapata watalii zaidi ya milioni 12 kwa mwaka, hii yote ni kwa sababu hatuna mashirika ya ndege ya kwetu."

"Kwa hiyo niwaombe tu Watanzania wapende mali zao, kwa sababu wakati mwingine nikiangalia mitandao na magazeti ni ajabu huwezi kuamini kama hao ni Watanzania, unakuta wanasifia tu ndege za watu wengine na wanazibeza za kwao."

MZOZO WA MPAKA KATI YA MALAWI NA TANZANIA WAIBUKA TENA

21:15 Add Comment

Ramani mpya iliyotolewa na Tanzania ambayo inaonyesha kuwa inaamiliki nusu ya Ziwa linalozozaniwa la Malawi au Nyasa, imezua mzozo mpya na Malawi ambayo inasema kuwa ramani hiyo sahihi.
Ramani ya Tanzania inaonyesha kuwa eneo la Kaskazini Mashariki mwa ziwa hilo ni sehemu ya himaya yake, lakini Malawi nayo inadai kuwa eneo hilo lote ni lake.
Malawi imeomba Umoja wa Mataifa, Mungano wa Afrika na mashirika mengine ya kimataifa kuingilia kati.
Msemaji wa wizara ya mashauri ya nchi za kigeni nchini Malawi, Rejoice Shumba amesema kuwa Malawi imeandika barua kwa mashirika makuu duniani ikiyataka kupuuzilia mbali ramani ya Tanzania.
Hii si mara ya kwanza Malawi imepinga ramani hiyo ya Tanzania.
Msukosuko uliibuka mwaka 2011 wakati Malawi ilianza shughuli za kutafuta mafuta kwenye ziwa hilo.
Serikali ya Tanzania bado haijatamka lolote kukuhusu suala hilo.
Nini hasa kinazozaniwa?
Fahari ya nchi na maswala ya kujiendeleza kiuchumi kwa Malawi na Tanzania kila mmoja akisimama kidete kusisitiza msimamo wake.
Kwa Tanzania, ziwa hilo linajulikana kama Nyasa, wakati nchini Msumbiji inajulikana kama Lago Niassa.
Malawi na Tanzania ni koloni za zamani za Uingereza wakati Msumbiji ilikuwa chini ya ukoloni wa Ureno. Uingereza iliichukua Tanzania kutoka kwa Wajerumani baada ya wao kushindwa katika vita vya kwanza vya dunia.
Kando na ripoti za kuwepo mafuta na gesi katika ziwa hilo, ziwa lenyewe ni kivutio kikubwa cha watalii.
Malawi inasema inashauriana na Msumbiji kuhusiana na uchimbaji wa mafuta katika siku za baadaye ili kuzuia mzozo wa kidiplomasia .
Je hii ni mara ya kwanza kwa mzozo huu wa ziwa Malawi kutokea?
Hapana. Mapema miaka ya sitini, Malawi ilidai umiliki wa ziwa hilo kwa kuambatana na makubaliano ya mwaka 1890 Heligoland kati ya Uingereza na Ujerumani ambayo yalisema kuwa mpaka kati ya nchi hizo uko upande wa Tanzania.
Makubaliano hayo yaliafikiwa na Muungano wa Afrika na Tanzania ikaitikia ingawa shingo upande. Mzozo mpya kati ya nchi hizo ukaripotiwa tena kati ya mwaka 1967 na 1968.
Ulichipuka tena mwaka mwaka 2011, Malawi ilipotoa leseni ya kuchimba mafuta kwa kampuni ya British Surestream Petroleum Limited. Sehemu iliyotolewa kwa uchimbaji wa mafuta ni sehemu yenye mraba wa kilomita 20,000 sehemu ambayo Tanzania inasema ni yake.
Vyombo va habari viliripoti mwezi Julai mwaka 2012 kuwa mitumbwi ya wavuvi na ya watalii kutoka Malawi ilivuka na kuingia upande wa Tanzania
Tanzania nayo ikasema kuwa ingetafuta ushauri kutoka jamii ya kimataifa ikiwa nchi hizo hazingeweza kusuluhisha mzozo huo zenyewe.
Hofu ya hatua za kijeshi
Hofu ya mzozo kutokota na kuwa mbaya zaidi ilijitokeza mwaka 2012 wakati Tanzania iliposema kuwa ingelinda mipaka yake na kuzingatia sheria za kimataifa.

MKUTANO SIMBA BADO NI MAJANGA

06:00 Add Comment

BARAZA la Wadhamini wa Simba limemwomba Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kusimamisha mkutano wa dharura wa mabadiliko ya Katiba uliopangwa kufanyika Desemba 11 kutokana na wao kutoshirikishwa chochote kama wenye mali.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa baraza hilo, Hamisi Kilomoni alipozungumza na waandishi wa habari jana akisema inaweza kuleta mpasuko ambao utakuwa na madhara kiusalama.
“Mkutano uliopita mliona Mwenyekiti Aveva akitolewa chini ya usalama wa askari hali iliyoonesha kuwa usalama ulikuwa mdogo, hivyo tunaomba mkutano wa Desemba 11, usifanyike hadi wanachama wahakikiwe,” alisema Mzee Kilomoni.
Pia Kilomoni alisema wamepokea barua kutoka kwa wanachama wakilalamikia mkutano huo ambapo nakala za barua zimefika hadi kwa Rais John Magufuli, Waziri Mkuu, Waziri wa Michezo, Baraza la Michezo (BMT) pamoja na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), hivyo kwa kuangalia kwa kina wanaiomba Serikali kusimamisha mkutano huo.
“Hapa kuna barua nyingi kutoka kwa wanachama kuomba kusitisha mkutano huo, mpaka kufikia kupeleka barua kwa Rais wa nchi ujue hilo sio suala dogo sisi kama wenye klabu tumeamua kumuomba Mkuu wa mkoa kuusimamisha ili isije ikatokea balaa zaidi,” alisema Kilomoni.
Aidha, Mzee Kilomoni alisema bado yeye yupo kwenye orodha ya wadhamini wanne wa klabu hiyo baada ya kupinga kuenguliwa kwenye mkutano mkuu wa wanachama uliofanyika Agosti mwaka 2014.
Kilomoni alithibitisha kwa kuonesha barua kutoka Rita iliyotolewa Agosti 12 mwaka huu ikianisha majina ya wadhamini wa klabu ya Simba, ambao ni Abdul Wahab Abas, Ally Sykes (marehemu), Ramesh Patel na yeye mwenyewe (Kilomoni).
Mkutano huo utakaofanyika Jumapili ijayo ni kwa ajii ya kupitisha mabadiliko ya Katiba ya Simba ili iweze kukidhi mchakato wa ubadilishaji umiliki wa klabu hiyo unaotaka kufanywa na mdau wa Simba Mohamed Dewji.
Tayari Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kupitia katibu wake Mohamed Kiganja ilishazuia mabadiliko hayo ya kiumiliki hadi pale Simba na Yanga zitakapobadilisha katiba zao kwanza.