UONGOZI wa Simba umesema unafanya mpango wa kumrejesha kikosini mshambuliaji wake wa zamani Emmanuel Okwi aliyevunja mkataba na klabu ya Sonderjyske ya Denmark.
Taarifa za kwenye mtandao wa klabu hiyo juzi ziliandika kwamba Okwi amefikia makubaliano ya kuvunja mkataba baada ya kukosa nafasi ya kucheza kwenye kikosi hicho.
Jana jioni Ofisa habari wa Simba, Haji Manara aliandika kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii: “Kocha Omog (Joseph- kocha mkuu wa Simba) ikimpendeza, Emmanuel Okwinho (Okwi) dimbani Feb 18, hiyo ndio habari mpasuko, ukinuna ongeza limao,”.
Simba inatarajia kucheza na Yanga katika mechi ya raundi ya pili ya Ligi Kuu baada ya kutoka sare ya bao 1-1 katika mechi ya kwanza.
Alipoulizwa na gazeti hili kuhusu taarifa hizo, Manara alikiri kuwa uongozi wake uko kwenye mchakato wa kumnasa mchezaji huyo na ikiwezekana atumike kwenye mechi zilizosalia za Ligi Kuu.
“Ni kweli tutamsajili kama mchezaji huru,” alisema.
Hata hivyo, tayari dirisha dogo la usajili kwa klabu za ligi limeshafungwa mpaka msimu ujao. Akilizungumzia hilo, ofisa habari wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas alisema Simba haiwezi kumtumia Okwi kwa sababu dirisha la usajili limeshafungwa.
“Ingewezekana kama usajili wa dirisha dogo ungekuwa haujafungwa, lakini dirisha limeshafungwa hivyo kama wanataka kumtumia, wasubiri mpaka usajili mwingine,” alisema.
Wakati wa usajili wa dirisha dogo Desemba mwaka jana Simba ilitaka kumsajili mshambuliaji huyo Mganda lakini ilishindwa baada ya klabu ya Sonderjyske kutaka ilipwe karibu sh milioni 240.
Hasimu wa Simba, Yanga pia ilijaribu kutaka kusajili mshambuliaji mwingine ili ashindane na Donald Ngoma baada ya kudaiwa kugoma kucheza kwenye mechi za kombe la Mapinduzi lakini ilishindikana kwa vile dirisha la usajili lilishafungwa.
Sonderjyske ilimsajili Okwi Julai 2015 kutoka Simba kwa mkataba wa miaka mitano uliotakiwa kumalizika mwaka 2020 ambapo tangu amesajiliwa Okwi alicheza mechi nne tu za Ligi Kuu ya Denmark na mbili za kombe la DBU ambapo alifunga mabao mawili.
Simba pia iliwahi kumuuza Okwi Etoile du Sahel ya Tunisia mwaka 2013 kwa dola za Marekani 300,000 kabla ya kusajiliwa na Yanga alipocheza kwa muda mfupi na kurejea Simba.
Okwi ni mshambuliaji kipenzi cha wanasimba kutokana na mafanikio aliyoipatia timu hiyo ambapo jana baada ya Manara kuweka suala lake kwenye mitandao ya kijamii, karibu mashabiki wengi wa soka walikuwa wakimzungumzia.
MATOKEO YA LEO YATAAMUA
MICHEZOMABINGWA watetezi wa Ligi Kuu bara, Yanga jana iliifunga Majimaji ya mjini hapa bao 1-0 katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja wa Majimaji na kujiongezea pointi tatu muhimu.
Matokeo hayo yanaifanya Yanga kufikisha pointi 43 pointi moja nyuma ya vinara Simba wenye pointi 44 ambao wanacheza leo na Mtibwa Sugar.
Aidha matokeo hayo pia yanaiweka pabaya Simba kwani sasa italazimika kushinda mechi yake ya leo kama inataka kuendelea kuongoza kwa tofauti ya pointi nne.
Yanga ilianza kulisakama lango la Majimaji mapema mwanzoni mwa mchezo huo ambapo katika dakika ya saba Simon Msuva nusura aandike bao lakini akiwa peke yake na kipa shuti lake lilipaa juu ya lango la Majimaji.
Bao la Yanga lilifungwa katika dakika ya 13 na Deus Kaseke aliyetumia vema makosa yaliyofanywa na kipa wa Majimaji, Aghton Antony aliyetema shuti la Msuva kabla mfungaji hajaliwahi na kuujaza mpira wavuni.
Kuingia kwa bao hilo kulizidisha ari kwa wachezaji wa Yanga ambao mwanzo walionekana kama kucheza kwa tahadhari na hivyo kuwabana zaidi wapinzani wao ambao nao walionekana kuwa na uwezo wa kurudisha bao hilo kutokana na mchezo waliokuwa wakicheza.
Hata hivyo, pamoja na jitihada za Majimaji hazikuzaa matunda na matokeo yake walikwenda mapumziko wakiwa nyuma ya bao 1-0 dhidi ya wageni wao.
Yanga ilianza tena mechi hiyo kwa kasi na dakika ya 48 Msuva tena akiwa kwenye nafasi nzuri ya kufunga, alipiga mpira nje.
Aidha mechi hiyo ilikuwa na rabsha za hapa na pale ambapo wachezaji wa Yanga kabla ya mechi kuanza na waligoma kuingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo wakidai kufanyiwa mambo ya kishirikina, kitendo ambacho walikifanya tena wakati wa mapumziko ambapo walibaki uwanjani wakigoma kuingia vyumbani.
Matokeo hayo yamezidi kuiweka pabaya Majimaji inayopambana kutoshuka daraja kwani imebaki katika nafasi yake ya 14 kwenye msimamo ikiwa na pointi 17.
Timu zilikuwa:
Yanga: Deogratius Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Haji Mwinyi, Andrew Vincent, Kelvin Yondani, Thaban Kamusoko, Simon Msuva, Haruna Niyonzima/Oscar Joshua, Amissi Tambwe, Juma Mahadhi na Deus Kaseke/Said Juma ‘Makapu.
Maji Maji: Agathon Anthony, Salehe Mohammed, Mpoki Mwakinyuke, Keneddy Kipepe, Bahati Yussuf/Emmanuel Semwanza, Yakoub Kibiga/Paul Nyangwe, Iddi kipwagile, Kelvin Kongwa, George Mpole, Hassan Hamisi na Lucas Kikoti/Peter Mapunda.
UGANDA YAPATA KIPIGO
MICHEZOAndre Ayew alifunga bao la pekee la mechi dhidi ya Uganda katika mechi ya ufunguzi ya kundi D katika michuano ya kombe la bara Afrika linaloendelea nchini Gabon.
Winga huyo wa klabu ya West Ham alifunga bao la penalti kunako dakika ya 32 baada ya nahodha Asamoah Gyan kuvutwa katika eneo la hatari.
Ghana pia ilitishia kupitia vichwa viwili vya Gyan ,huku Ayew na Christian Atsu wakimjaribu kipa wa Uganda Denis Onyango.
Uganda walikaribia lango la Ghana baada ya Faruku Miya kupiga mwamba wa goli lakini hawakuweza kusawazisha.
Uganda wanaocheza kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1978 hawakuwa na bahati.
Cranes walitengeza fursa chache na walishindwa kuingia katika lango la Ghana ambao walifurahia kulinda lango lao .
HUU NDIO MTEREMKO WA TAIFA STARS KUFUZU AFCON 2019
MICHEZOALIYEKUWA Kocha wa timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’, Charles Mkwasa amesema kilio chake kimesikika na hatimaye Tanzania imepangwa kwenye kundi rahisi kuwania kufuzu Kombe la Mataifa Afrika mwaka 2019.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mkwassa ambaye ameifundisha Taifa Stars akirithi mikoba ya kocha Mdenishi Mart Nooij amesema timu ambazo zipo kundi moja na Tanzania ni rahisi ukilinganisha na kundi la msimu uliopita ambapo ilipangwa na Nigeria na Misri.
“Timu zilizopangwa kundi moja na Tanzania ni timu za kawaida ukilinganisha na Misri au Nigeria, lakini maandalizi ya mapema ni muhimu ili kufanya vizuri,” alisema Mkwassa.
Pia Mkwassa alisema pamoja na kuonekana kuwa rahisi lakini kitendo cha nchi hizi kuwa na viwango vinavyokaribiana kinaweza kufanya iwe ngumu zaidi kwa maana ya kukamiana.
“Jukumu linabaki kwa Shirikisho la Soka (TFF), wachezaji pamoja na benchi la kiufundi kujiandaa kwani nilisema hadharani tumekuwa tukipangwa kwenye kundi la kifo ila droo ya sasa CAF walisikia kilio changu na inawezekana iwapo tutaamua,” alisema Mkwassa.
Tanzania imepangwa Kundi L pamoja na vinara wa soka ukanda wa Afrika Mashariki Uganda, Lesotho na Cape Verde, ambapo wengi wanasema ni jepesi ukilinganisha na huko nyuma iliyokuwa ikipangwa Stars.
Kwa upande wa timu ya Taifa ya Kenya 'Harambee Stars' ambayo ipo ukanda huu wa Afrika Mashariki imepangwa kundi F sambamba na Ghana, Ethiopia na Sierra Leone.
Msemaji wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas alisema ratiba hiyo ni faraja kubwa kwa Tanzania kwani wadau wa soka wakiungana na TFF, “hakuna shaka tunaweza kufuzu kwa fainali hizo za 2019.”
Hata hivyo,Lucas alisema pamoja na kuwepo katika kundi linaloonekana jepesi, lakini bado maandalizi ya Stars yanatakiwa kuwa makubwa kwani Uganda na Cape Verde bado ni timu nzuri.
Alisema kuwa Uganda Cranes ni timu nzuri na itakuwa na hamu kubwa ya kucheza tena fainali hizo za mwaka 2019 baada ya kushiriki zile za mwaka huu nchini Gabon, ambazo zinaanza leo.
Wenyeji wa michuano hiyo Cameroon ambayo imefuzu moja kwa moja imepangwa kundi B pamoja na Morocco, Malawi na mshindi kati ya Comoro na Mauritius.
Wakati huo huo timu za Sao Tomé, Madagascar, Comoro, Mauritius, Djibouti na Sudan Kusini wataanzia kwenye mechi za mtoano Machi na mataifa matatu yataingia kwenye hatua za makundi.
Jinsi makundi yalivyopangwa:
Kundi A: Senegal, Equatorial Guinea, Sudan, Sao Tome/Madagascar
Kundi B: Cameroon, Morocco, Malawi, Comoro/Mauritius
Kundi C: Mali, Gabon, Burundi, Djibouti/Sudan Kusini.
Kundi D: Algeria, Togo, Benin Gambia.
Kundi E: Nigeria, Afrika Kusini, Libya, Shelisheli.
Kundi F: Ghana, Ethiopia, Sierra Leone, Kenya.
Kundi G: DR Congo, Congo Brazzaville, Zimbabwe, Liberia.
Kundi H: Ivory Coast, Guinea, Jamhuri ya Afrika ya kati, Rwanda
Kundi I: Burkina Faso, Angola, Botswana, Mauritania.
Kundi J: Tunisia, Misri, Niger, Swaziland.
Kundi K: Zambia, Msumbiji, Guinea-Bissau, Namibia.
Kundi L: Cape Verde, Uganda, Tanzania, Lesotho.
NGASA ACHAMBUA UDHAIFU WA YANGA
MICHEZOKIUNGO mshambuliaji wa zamani wa Yanga anayechezea Mbeya City, Mrisho Ngassa amesema Yanga inahitaji wachezaji wawili wa kuchezesha timu ili kuwa na uwiano mzuri.
Akizungumza na gazeti hili, Ngassa alisema Yanga inahitaji wachezaji wenye uwezo wa kuuchezea mpira na kutoa pasi za mwisho.
“Ukiangalia Yanga wanavyocheza kwa sasa, unaona kabisa inakosa watu wa kuchezea mpira na kutoa pasi za mwisho kama alivyo Haruna Niyonzima ili wawe na uwiano mzuri katika timu, lazima wawapate hao watu,”alisema Ngassa.
Pia Ngassa alisema sababu hiyo ndio chanzo cha Yanga kufanya vibaya katika mchezo wa Kombe la Mapinduzi dhidi ya Simba.
“Mechi ilikuwa nzuri, Simba waliwazidi Yanga katikati kwani walikuwa wanacheza mipira mirefu kumtumia Msuva peke yake, hivyo Simba wakagundua njia hiyo, baada ya kusogea pembeni wakaua mipango ya Yanga,” alisema Ngassa.
Ngassa alisema wachezaji wengi wa Yanga kwa sasa wamechoka baada ya kucheza michezo mingi ya kimashindano, hivyo miili yao inahitaji kupumzika.
AZAM FC MAPINDUZI CUP CHAMPIONS
MICHEZOZanzibar. Shuti la ‘mwendokasi’ la umbali usiopungua mita 25 la kiungo Himid Mao limetosha kuamua matokeo ya mchezo wa Fainali ya Mapinduzi uliofanyika mjni Zanzibar.
Miamba hiyo ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliichapa Simba bao 1-0 na kutosha kutangazwa mabingwa wapya wa Kombe la Mapinduzi.
Wakinolewa na kocha wa vijana wa Azam, Idd Cheche aliyechukua kwa muda mikoba ya Zeben Hernandez aliyetimuliwa kwa matokeo mabaya, Azam FC iliibuka na ushindi wa bao la dakika ya 13 lililofungwa na kiungo huyo wa Taifa Stars, Himid.
Ushindi huo pia umeifanya Azam FC kutwaa taji la tatu la Kombe la Mapinduzi baada ya awali kulitwaa miaka ya 2011 na 2012.
Katika mashindano hayo, beki wa Simba, Method Mwanjali amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa Mapinduzi Cup, tuzo ya kipa bora imekwenda kwa Aishi Manula wa Azam FC, timu bora ya vijana ni Taifa Jang’ombe.
Mfungaji bora ni kiungo wa Yanga, Saimon Msuva, aliyeweka kimiani mabao manne, wakati mwamuzi bora wa mashindano hayo akichaguliwa kuwa Mfaume Ali.