MAHASIMU wa jadi Simba na Yanga zinatarajiwa kushuka dimbani Februari 18 katika mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu Tanzania bara.
Katika mchezo wa raundi ya kwanza ambao ulimalizika kwa vurugu huku mabomu ya machozi yakirindima, mageti kuvunjwa na viti kung’olewa na mashabikii wa Simba kwa hasira baada ya bao la mshambuliaji Mrundi Amis Tambwe, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.
Tambwe kabla hajafunga bao hilo alishika mpira na mkono, jambo lililoibua vurugu hizi zilizosababisha serikali kuzipiga marufuku Simba na Yanga kutumia uwanja huo.
Hata hivyo wiki iliyopita Yanga ilisaini mkataba na serikali kwa ajili ya kuutumia uwanja huo ambapo imepewa masharti ya kufidia chochote kitakachoharibiwa uwanjani hapo.
Mzunguko wa pili wa ligi umepangwa kuanza Desemba 17 mwaka huu na tayari timu zimeanza kujiandaa huku Simba ikienda kujichimbia Morogoro na Yanga ikitarajiwa kwenda Pemba kwa maandalizi.
Katika mzunguko huo, Yanga itakuwa chini ya kocha mpya Mzambia George Lwandamina na itaanza harakati zake za kutetea taji kwa kumenyana na JKT Ruvu kwenye uwanja wa Uhuru wakati Simba ikiwa ugenini kumenyana na Ndanda katika uwanja wa Nang’wanda Sijaona Mtwara.
Simba inaongoza ligi ikiwa na pointi 35 pointi mbili mbele dhidi ya mahasimu wao Yanga ambao wamepania kutetea kwa mara ya tatu ubingwa wa Ligi Kuu bara. Kocha Lwandamina anataka mchezo mmoja wa kirafiki kabla ya ligi ili kuwajua vizuri wachezaji baada ya kurithi timu kwa Mholanzi Hans van der Plujim mwezi uliopita.
Pluijm sasa ni Mkurugenzi wa Ufundi wa Yanga. Kikosi hicho kinafanya mazoezi kwenye uwanja wa Gymkhana Dar es Salaam.
Kwa upande wa Simba, kocha Mcameroon Joseph Omog anaonekana kuvutiwa zaidi na kambi ya Morogoro baada ya kujificha huko kwa maandalazi ya mwanzoni mwa msimu na amependekeza timu irudi huko.
Simba inatarajiwa kuwa na mabadiliko ya kipa langoni ambapo sasa huenda akaonekana Mghana Daniel Agyei aliyesaini mwaka mmoja kucheza kwa klabu hiyo ya Msimbazi.
Mechi nyingine zitakazochezwa Desemba 17 ni Mbeya City dhidi ya Kagera Sugar, Ruvu Shooting dhidi ya Mtibwa Sugar wakati Mwadui ikicheza na Toto Africans. Ligi hiyo itaendelea tena Desemba 18 kwa Simba kucheza na Ndada, huku Mbao ikimenyana na Stand United wakati African Lyon ikicheza na Azam, Prisons na Maji maji.
Next
« Prev Post
« Prev Post
Previous
Next Post »
Next Post »
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
EmoticonEmoticon