MECHI ZA KIMATAIFA ZAIREJESHA YANGA TAIFA

06:08

Siku chache baada ya Serikali kuirejeshea Yanga ruhusa ya kutumia uwanja wa Taifa, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye ameeleza sababu za kuirejesha timu hiyo uwanja huo na ukomo wa makubaliano yao.
Kurejeshwa kwa Yanga uwanjani humo kuliacha maswali ambayo jana Waziri Nape aliyatolea ufafanuzi ikiwamo muda wa makubaliano ya Serikali na Yanga, gharama na namna Yanga itakavyoulipia uwanja huo na kwa nini Yanga pekee ndiyo imerejeshwa.
Kabla ya kuirejesha Yanga, Serikali iliifungia timu hiyo sanjari na Simba kufuatia mashabiki wa timu hizo kung’oa viti na kuvunja mageti ya uwanja kwenye mchezo baina ya timu hizo uliofanyika Oktoba Mosi.
Akizungumza na gazeti hili jana, Waziri Nape alisema ina kila sababu ya kuirejesha Yanga kutumia Uwanja wa Taifa.
“Yanga inashiriki mashindano ya kimataifa, kama tungeendelea kuizuIa ingekuwa na wakati mgumu kwenye mashindano hayo kwani uwanja ambao Fifa (Shirikisho la Soka la Kimataifa) na lile la Afrika (CAF) linautambua kwa Tanzania bara ni ule,” alisema.
Akizungumzia ukomo wa makubaliano yao na Yanga kutumia uwanja huo, Waziri Nape alieleza kuwa ni hadi pale Yanga itakapomaliza mechi zake za kimataifa, huku akifafanua kuwa endapo malipo ya uwanja huo yatatokana na viingilio vya mlangoni au mapato mengine ya klabu. “Gharama za malipo kuna utaratibu ambao tunauandaa, ukikamilika tutauweka wazi,” alisema na kuongeza:
“ Kuhusu timu nyingine, hasa Simba kurejea kuutumia uwanja huo, hakuna timu nyingine itakayoruhusiwa zaidi ya Yanga hadi ukarabati wa uwanja huo utakapokamilika.
“Tutaangalia kwa timu nyingine baada ya ukarabati unaoendelea kukamilika kama tutaziruhusu kutumia uwanja huo au la.”

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »