WANAFUNZI 21 WASIMAMISHWA MASOMO BAADA YA KUKUTWA NA UJAUZITO

06:36
Katika kipindi cha miezi tisa ya mwaka huu, wanafunzi 21 wa sekondari katika Halmashauri ya Mji wa Kahama, wamekatisha masomo baada ya kupata ujauzito.
Ofisa Elimu Sekondari wa Halmashauri hiyo, Anastasia Manumbu amezitaja shule ambazo wanafunzi wake wamekatisha masomo kwa ujauzito kuwa ni Abdurahim, Seeke, Kishimba, Nyasubi, Nyihogo, Bukamba, Mwendakulima na Nyashimbi.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kahama, Anderson Nsumba amesema uongozi wake umeanzisha utaratibu wa kuwapima ujauzito wanafunzi wote wa kike kila baada ya miezi mitatu.
“Upimaji huu ni kwa wanafunzi wa shule zote za msingi na sekondari na tunachukua hatua za kisheria dhidi ya wote wanaobainika kuhusika kwa njia moja au nyingine na ujauzito,” amesema Nsumba.
Kwa mujibu wa utafiti dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia uliofanywa na Chama cha Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (Shdepha+) Tawi la Kahama, baadhi ya wanafunzi walipata ujauzito kwa kubakwa au kurubuniwa kwa kupewa fedha.
Mkurugenzi wa Shdepha+ Kahama, Venance Mzuka amesema chama hicho kimeanza kuwajenga kisaikolojia wanafunzi hao ili warejee kuendelea na masomo shuleni na kutimiza ndoto zao baada ya kujifungua.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »