LIGI KUU BARA LEO

07:17

SIMBA, Yanga na Azam FC leo zitashuka kwenye viwanja tofauti kusaka pointi tatu ambazo zitaendelea kuwapa nafasi ya kuendelea kuingia katika vita ya ubingwa, kila moja ikionesha shauku na umuhimu wa kushinda ugenini.
Vinara wa ligi hiyo Wekundu wa Msimbazi watakuwa kwenye Uwanja wa Uhuru dhidi ya African Lyon, wakijivunia kushika usukani wa ligi kwa pointi 35 na kuziacha Yanga na Azam kwa tofauti ya pointi nane hadi 13.
Simba haijapoteza mchezo hata mmoja katika mechi 13 ilizocheza, ikishinda 11 na kupata sare mbili. Mbali na rekodi hiyo bora, pia ndio timu yenye mchezaji anayeongoza kwa ufungaji Shiza Kichuya akiwa na mabao tisa.
Timu hiyo ina nafasi kubwa ya kushinda mchezo wa leo baada ya kutoka kushinda dhidi ya Stand United bao 1-0, uliochezwa Shinyanga hivi karibuni. Inacheza na African Lyon ambayo licha ya kutokuwa katika nafasi nzuri bado haipaswi kudharauliwa kwa kuwa haitabiriki.
Timu hiyo ina pointi 14 katika michezo 14 iliyocheza ikishika nafasi ya 11 kwenye msimamo. Yanga itakuwa kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya. Mabingwa hao watetezi wanashika nafasi ya pili kwenye msimamo wakiwa na pointi 27 katika michezo 13 iliyocheza.
Mchezo wa leo una umuhimu mkubwa kwao kushinda kama wanataka kukimbizana na Simba katika mbio za ubingwa. Mchezo huo hautakuwa rahisi kwa kila timu, kwani zote zimetoka kupoteza michezo yao iliyopita Yanga ikifungwa mabao 2-1 na Mbeya City na Prisons ikifungwa na Ndanda FC bao 1-0.
Kuanzia msimu wa mwaka 2013 hadi sasa, Yanga imekuwa na rekodi nzuri dhidi ya Prisons, lakini Februari mwaka huu katika mechi ya mzunguko wa pili ya ligi ya msimu uliopita kwenye Uwanja wa Sokoine, timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2. Azam FC itakuwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza ikichuana na Mbao FC.
Timu hii imeanza kurudi taratibu baada ya kushinda michezo miwili iliyopita ya ugenini. Iliifunga 1-0 Toto Africans na 3-2 Kagera Sugar. Katika michezo 13 iliyocheza imeshinda sita, sare nne na kufungwa mitatu ikishika nafasi ya 13 kwa pointi 22. Inakutana na Mbao FC ambayo imekuwa ikizikazia timu kubwa kila inapokutana nazo.
Mbao licha ya kutokuwa na uzoefu wa kutosha wa ligi, inapokutana na timu kubwa hucheza mchezo mzuri wa kujihami na kushambulia mara chache na mara unapoidharau ni rahisi kuabisha kwani ina wachezaji wanaojituma.
Timu hii bado haiko katika nafasi nzuri baada ya kupoteza michezo kadhaa iliyopita ikiwa ugenini. Inashika nafasi ya tatu kutoka mwisho, ikiwa na pointi 12 katika michezo 14. Ndanda FC inayoshika nafasi ya 10 kwa pointi 16 itaikaribisha Stand United kwenye uwanja wake wa nyumbani Nangwanda Sijaona Mtwara.
Huu utakuwa mchezo mgumu kwa kila timu kwani timu hiyo ya Mtwara ni mara chache kufungwa kwenye uwanja wake msimu huu. Pia, Stand ni timu ambayo imekuja kivingine, iko vizuri na kwa sasa inashika nafasi ya nne,ikiwa na pointi 22 katika michezo 14 iliyocheza.
Ni mchezo ambao iwapo Stand itakubali kichapo itaendelea kushuka kwenye msimamo na kutoa nafasi kwa timu za chini yake kupanda. Kagera Sugar itakutana na Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Kaitaba.
Kagera inashika nafasi ya tano ikiwa na pointi 21 na Ruvu nafasi ya saba kwa pointi 19. Kila mmoja anahitaji ushindi kujisogeza kutoka safasi moja hadi nyingine. JKT Ruvu itaikaribisha Toto Africans.
Timu zote mbili zinafuatana kwa kushika mkia wakitofautiana kwa pointi moja. JKT ina pointi 12 na Toto 11 wote wakiwa wameshacheza michezo 14. Hii ni mechi inayohitaji ushindi kwa kila mmoja kujiondoa katika nafasi walizopo.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »