JUMUIYA YA WANAFUNZI YAIPA SERIKALI SIKU SABA

07:14

Dar es Salaam. Jumuiya ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Tanzania (Tahliso), imeikomalia Serikali ikitaka wote wanaostahili kulipwa walipwe ndani ya wiki moja.
Kauli hiyo ya Tahliso imekuja kutokana kuwapo kwa malalamiko mengi ya wanafunzi kukosa mikopo.
Akizungumza baada ya majadiliano na viongozi wa vyuo 44 vikuu nchini, mwenyekiti wa Tahliso, Stanslaus Kadugalize amesema wamekubaliana kuwa Serikali ihakikishe baada ya siku saba iwe imewapa mikopo wanafunzi wenye sifa.
Amesema mwaka huu wanafunzi wachache wamepata mkopo,
hivyo Serikali iongeze bajeti ili kuwanufaisha wenye sifa stahiki.
Ameitaka wizara husika kwa kushirikiana na mamlaka wanazofanya kazi wawashughulikie viongozi waliowapa mikopo wanafunzi wanaodhaniwa kutokuwa na sifa.
Kadugalize ametaja jambo jingine walilokubaliana katika mkutano uliofanyika Dar es Salaam jana, kuwa ni pamoja na kuondoa dodoso wanazotakiwa kujaza wanafunzi wa mwaka wa pili na wa tatu.
“Waliokosa mikopo wote walijaza fomu za kuomba, hivyo taarifa zao wanazo, warudi wakazitazame na kisha wawape mikopo. Kukata rufaa ni kuwasumbua na kuwaonea,” amesema Kadugalize.
Waziri wa Mikopo wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustine cha Mwanza, Ayo Emmanuel amesema wanaitaka bodi kulipa deni la Sh1.7 bilioni za ada kwa wanafunzi waliopata mkopo mwaka 2015/16.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELSB), Abdul Razaq Badru amesema wametoa siku 90 kwa wanafunzi wenye sifa za kufanya marekebisho na kuanzia leo na kesho watatoa majina mengine ya wanafunzi waliokata rufaa ili zifanyiwe kazi.
Amesema Serikali inafanya kazi kwa bajeti na mipango, hivyo mipango inayotekelezwa sasa ni ile iliyopangwa.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »