Dar es Salaam. Kama Rais John Magufuli amepania kufanyia kazi nyufa alizozitaja Mwalimu Julius Nyerere miaka 21 iliyopita, ana kazi kubwa zaidi ya hiyo kwa mujibu wa wasomi walioongea na Mwananchi katika kumbukumbu ya kifo cha muasisi huyo wa Taifa.
Wanazuoni hao wanaona Taifa linakumbwa na nyufa zaidi ya alizoziacha Mwalimu Nyerere, wakati zile alizozitaja zikiendelea kutopata ufumbuzi.
Katika hotuba maarufu ya Juni 14, 1995, Mwalimu Nyerere alitaja ubaguzi, kutojali utawala wa sheria na rushwa kuwa ni nyufa zilizokuwa zinalikabili Taifa wakati likielekea kwenye uchaguzi wa kwanza tangu kurejeshwa kwa vyama vingi.
Alisema ubaguzi baina ya Watanganyika na Wazanzibari ni hatari kwa nchi, wakati kutoheshimu katiba na sheria za nchi ni tatizo jingine hali kadhalika rushwa katika kupata viongozi.
Tangu aingie madarakani, Rais Magufuli ameonyesha nia ya kufuata nyayo za muasisi huyo wa Taifa kwa kupambana na rushwa na uovu mwingine kwenye Serikali yake.
Lakini wakati wasomi hao waliohojiwa na Mwananchi wanaona mambo hayo hayajashughulikiwa kikamilifu kuziba nyufa na badala yake mambo zaidi yanaibuka miaka 17 baada ya kifo chake.
“Ingawa nchi bado ina umoja alioujenga Mwalimu, kuna dalili za kumomonyoka maadili, kama tishio jipya la ukanda,” alisema Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu).
Msomi huyo alisema Mwalimu aliacha taifa moja, lakini hivi sasa limeanza kugawanyika kikanda na kiitikadi.
Profesa Mpangala alisema uadilifu ulianza kutoweka tangu wakati Mwalimu akiwa hai na ndiyo maana katika baadhi ya hotuba zake za mwisho kabla ya kufariki dunia alikuwa akilizungumzia sana suala hilo.
Profesa Mpangala alisema kumzungumzia Mwalimu kwa kujivunia bila kutekeleza unayoyasema, ni kulitumia vibaya jina lake.
Alisema njia sahihi ya kumtaja ni kukemea aliyoyakataa na kutumia njia hiyo kama Dira ya Taifa ambayo itatumika kuongoza kwa haki na usawa.
“Turudi kwenye umoja, mshikamano, kuheshimiana, kuthaminiana, hapo nchi itarudi ilikotoka na hali itakuwa ya kawaida,” alisema.
Mtazamo wa Profesa Mpangala unalingana na Profesa Bashiru Ally aliyesema kuwa mbali ya nyufa alizozitaja Mwalimu Nyerere, ziko mpya ambazo ni hatari zaidi, akitaja ongezeko la tofauti kati ya walionacho na maskini.
Alisema kibaya zaidi pengo hilo linajengwa na watumishi wa umma, ambao alisema wamekuwa wakijilimbikizia mali.
Alifafanua kuwa katika hili hakuna usawa na nchi ikikosa usawa ni vigumu kuwa na jamii ya haki, hivyo watu watatafuta kujilinda kwa kutumia dini zao, makabila yao, elimu zao na vyeo vyao.
“Naunga mkono kauli ya (Rais Mstaafu, Ali) Mwinyi (aliyesema hivi sasa hakuna uadilifu na kuwepo kwa udini na ukabila) na (Jaji Joseph) Warioba (aliyesema nchi inaendeshwa kwa matukio),” alisema Bashiru.
“Na bado hawajasema vya kutosha, wajitokeze waseme. Haya masuala yanatakiwa kujadiliwa, hivyo wakitoka na kuzungumza wataibua mjadala. Tofauti na hayo, nyufa alizozitaja mwalimu Nyerere litazidi zaidi ya hapa.”
Alieleza sasa hali ni mbaya zaidi kwa sababu kuna matatizo kama kutosimamia sheria na kutofuata Katiba katika kuongoza nchi.
Next
« Prev Post
« Prev Post
Previous
Next Post »
Next Post »
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
EmoticonEmoticon