SIMBA imeachana na kipa wake Vincent Angban wa Ivory Coast na kiungo wa Congo DR, Mussa Ndusha.
Dirisha dogo la usajili linafungwa leo ambapo Simba kama zilivyo timu nyingine zinazoshiriki Ligi Kuu imefanya marekebisho kwenye kikosi chake kujiimarisha na mzunguko wa pili wa ligi unaotarajiwa kuanza mwishoni mwa wiki hii.
Habari kutoka Simba zinasema benchi la ufundi chini ya kocha Mcameroon Joseph Omog limeamua kuachana na Angban kwa vile nafasi yake imezibwa na kipa Mghana Daniel Agyei aliyesaini mkataba wa mwaka mmoja.
Angban amedaka kwa mafanikio Simba katika mzunguko wote wa kwanza akidaka mechi zote za timu hiyo iliyopoteza mechi mbili tu kati ya 15.
Aidha katika kujiimarisha, Simba imesaini mkataba wa mwaka mmoja na kiungo Mghana, James Kotei na Juma Luizio aliyekuwa akichezea Zesco United ya Zambia pamoja na mshambuliaji wa Stand United, Pastory Athanas.
Wachezaji wengine wa kigeni Simba ni Janvier Bokungu wa Congo DR, Method Mwanjali (Zimbabwe), Juuko Murshid (Uganda) na washambuliaji Laudit Mavugo (Burundi) na Frederick Blagnon (Ivory Coast). Msemaji wa Simba, Haji Manara alipoulizwa kuhusu usajili huo alisema taarifa za kila kitu atazitoa leo.
“Tupo kwenye usajili na dirisha linafungwa kesho (leo) hivyo tulieni kila kitu kitasemwa kesho,” alisema.
Wakati huo huo, kocha msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja amesema sasa wapinzani waje kwani wamejipanga kuendeleza kichapo kwa kila aliyeko mbele yao kuhakikisha wanatimiza malengo yao ya kutwaa taji la ligi.
Mzunguko wa pili wa Ligi Kuu unaanza mwishoni mwa wiki hii, na Simba ambayo ndio vinara kwa tofauti ya pointi mbili, wataanza kampeni zao Jumapili kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona Mtwara wakipambana na Ndanda. Simba inatarajiwa kuelekea Mtwara leo kwa ajili ya mechi yao hiyo.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mayanja alisema wamejipanga vizuri na wako tayari kuanza mechi kuelekea kwenye mafanikio.
“Tumejipanga vizuri na wachezaji wote wanaendelea vizuri. Tunatarajia kuondoka kesho (leo) kuelekea Mtwara kuanza safari yetu ya kuendeleza ushindi kwenye mechi za kukamilisha msimu,” alisema.
Kocha huyo Mganda alisema wamekamilika kwa kila kitu, na wameridhika na viwango vya wachezaji wapya. “Tumewaona wachezaji wote hawana tabu, wako vizuri, tunategemea watafanya vizuri zaidi,” alisema.
Alihimiza mashabiki wa klabu hiyo kuendelea kuwaunga mkono kama ilivyokuwa kwa mechi za mzunguko wa kwanza ili kutimiza ndoto zao za kuchukua ubingwa. Simba ndio kinara kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 35 ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 33 na Azam FC pointi 25.
Next
« Prev Post
« Prev Post
Previous
Next Post »
Next Post »
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
EmoticonEmoticon