VIONGOZI WA AFRIKA WAMEJIFUNZA NINI KUTOKA UCHAGUZI WA MAREKANI

06:14

Uchaguzi wa kumpata Rais wa 45 wa Marekani ulikamilika wiki iliyopita kwa mwanasiasa ‘mropokaji’ na mgombea wa Chama cha Republican, Donald Trump kuibuka kidedea dhidi ya Hillary Clinton wa Democratic ambaye ulimwengu mzima ulitarajia angeibuka mshindi.
Trump ataapishwa Januari 20, 2017 na kumrithi Rais Barack Obama. Ulikuwa uchaguzi hasa kwa maana ya kukidhi viwango vya demokrasia. Kila idara au taasisi ilitimiza wajibu kwa uhuru na kuhakikisha Taifa hilo lenye nguvu za kijeshi na kiuchumi linapata kiongozi wake.
Uzuri ni kwamba Marekani ni taifa lililojengwa kwa misingi ya kila taasisi kufanya kazi kwa uhuru bila kuingiliwa na mamlaka yoyote. Wanataaluma wa sayansi ya siasa wana usemi kuwa “Uchaguzi Mkuu ndiyo mchakato wa juu kabisa na kipimo halisi cha ukomavu wa demokrasia katika taifa linalofuata misingi ya haki na utawala bora.”
Hiki ndicho walichofanya Wamarekani kwa kuchagua kiongozi wao na kinachosubiriwa ni kutimiza aliyoahidi.
Usemi kwamba uchaguzi mkuu ni mchakato wa juu wa kidemokrasia katika taifa lolote ulimwenguni umenitafakarisha hasa nikiangalia namna mataifa ya Afrika yanavyojikongoja katika kukuza demokrasia na utawala bora.
Unanifikirisha kwa namna ninavyoshuhudia na kufuatilia chaguzi katika mataifa mbalimbali barani Afrika. Mwaka 2015 mataifa kadhaa ya Afrika yalichagua viongozi wao ikiwamo Tanzania ambayo ilishuhudia John Magufuli akitawazwa kuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano kwa ushindi wa asilimia 58 dhidi ya mpinzani wake wa karibu, Edward Lowassa aliyevuna asilimia 39.
Kama nilivyosema hapo awali, uchaguzi ndiyo kipimo cha ukuaji wa demokrasia katika taifa linalofuata misingi ya utawala bora. Kufutwa kwa uchaguzi wa Zanzibar licha ya kulalamikiwa na jumuiya za ndani, kikanda na kimataifa kulitia doa Tanzania, taifa linalosifika miongoni mwa mataifa ya kiafrika kwa kudumisha amani na utulivu.
Kuna mataifa ambayo yanatarajiwa kufanya uchaguzi wake mkuu mwishoni mwa mwaka huu na mwakani. Baadhi ya mataifa hayo ni Gambia ambayo itafanya uchaguzi Desemba Mosi na Ghana itafanya Uchaguzi Mkuu Desemba 7, mwaka huu.
Kenya na Rwanda, mataifa jirani na Tanzania yanatarajia kufanya uchaguzi mwakani hatua ambayo itakuwa kipimo kingine cha demokrasia.
Mtafiti John Campbell kutoka taasisi ya Coucil on Foregn Relation katika chapisho lake liitwalo ‘African Democracy:Elections Despite Divison’ amesawiri migawanyiko inayosababishwa na wanasiasa inavyovuruga mchakato wa uchaguzi katika mataifa mengi barani Afrika.
Ametoa mifano ya namna wanasiasa katika mataifa ya Ivory Coast, Nigeria na Kenya walivyowagawa wananchi katika misingi ya kidini, kikabila, kikanda na kutumia taasisi za kiusalama kufanikisha mipango yao ya kutwaa madaraka katika uchaguzi.
Ninakubaliana na Campbell, mataifa ya Kenya, Rwanda, Gambia, Ghana na DRC yanatarajia kufanya chaguzi lakini matatizo ni yaleyale ya miaka nenda rudi.
Mamia kwa maelfu ya raia waliuawa katika mataifa ya Ivory Coast, Burundi na Burkinafaso baada ya viongozi kutokuwa tayari kuruhusu wananchi wawahukumu kupitia uchaguzi.
Rais wa Gambia, Yahya Jammeh kabla hata uchaguzi haujafanyika Desemba mwaka huu ametangaza haitaji ushauri wa mtu yeyote kuongoza taifa hilo, bali atamsikiliza Mwenyezi Mungu pekee. Jammeh aliyeingia madarakani mwaka 1994 kwa njia ya mapinduzi alitangaza kuwa Mungu akimjalia afya atalitawala taifa hilo kwa miaka bilioni moja.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »