PLUIJM AKUBALI KUBAKI YANGA KAMA MKURUGENZI WA BENCHI LA UFUNDI

07:34

Kocha wa Yanga, Mholanzi Hans van der Pluijm amekubali kubaki klabuni kama Mkurugenzi wa Ufundi na ndiye atamshauri kocha mpya, George Lwandamina kuhusu muundo wa benchi la Ufundi.
Kuna uwezekano mkubwa waliokuwa Wasaidizi wa Pluijm ndiyo wakawa wasaidizi wa Lwandamina pia, kwa kuwa wote bado wana mikataba na hakuna shaka juu ya utendaji wao.
Pluijm anaondoka Jangwani baada ya kuiongoza Yanga katika jumla ya mechi 128, akishinda 80, sare 25 na kufungwa 23.
Katika mechi 19 za nusu msimu mwaka 2014, alishinda 11, sare sita na kufungwa mbili, wakati katika mechi 110 za tangu mwaka jana, alishinda 69, sare 19 na kufungwa 21.
Msimu uliopita ulikuwa mzuri zaidi kwake, akibeba mataji yote matatu, Ngao ya Jamii, Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation (ASFC).
Pluijm pia aliiwezesha Yanga kufika hatua ya makundi ya michuano ya Afrika (Kombe la Shirikisho) kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1998 na mara ya pili kihistoria. Yanga ilifika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho mwaka huu baada ya mwaka 1998 kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa.
Msim uliopita Pluijm alishinda tunzo ya kocha bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »