WAZIRI MKUU AKARIBISHA WAWEKEZAJI

06:56

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi saba barani Afrika ambazo uchumi wake unakua kwa kasi, hivyo amewakaribisha wawekezaji kwenye sekta mbalimbali.
Majaliwa amesema Tanzania ni nchi ya pili kwa kasi ya ukuaji uchumi barani Afrika na kwamba, uchumi wake unakua kwa asilimia saba. Nchi inayoongoza ni Ivory Coast kwa asilimia 8.5, Senegal asilimia 6.6, D’jibout asilimia 6.5, Rwanda asilimia 6.3, Kenya asilimia 6.0 na Msumbiji asilimia 6.0.
Waziri Mkuu alitoa kauli wakati akifungua kongamano la Jumuiya ya Dawood Bohora lililohusu fursa za uwekezaji, kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Nyerere.
“Tanzania ina sera nzuri za uchumi ambazo zimesababisha kuendelea kuwa imara kwa zaidi ya miongo miwili sasa. Naikaribisha Jumuiya ya Bohora kuwekeza na kufanya biashara Tanzania,” alisema.
Alisema kampuni zitakazowekeza nchini zitafaidika na uwapo wa malighafi za kutosha, sera nzuri za uwekezaji na uhakika wa usalama wa mali kwa sababu ya hali ya amani na utulivu iliyopo.
Majaliwa amesema licha ya Tanzania kuwa na maeneo mazuri kwa uwekezaji, ina soko la uhakika kwa sababu ya kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (Sadc) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zenye watu takriban milioni 600.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »