Serengeti. Mikakati ya Serikali ya kukomesha vitendo vya ukeketaji wilayani hapa Mkoa wa Mara inayotarajiwa kuanza Desemba, imesababisha wazee wa kimila kushikwa kigugumizi kutangaza tarehe rasmi ya kuanza.
Desemba kila mwaka unaogawanyika kwa mbili huwa kunafanyika ukeketaji, wazee wa mila hutangaza tarehe mapema kwa ajili ya maandalizi.
Mwenyekiti wa koo ya Inchugu, Kabila la Wakurya kwa Tanzania na Kenya, Masonoro Marwa akizungumza na gazeti hili kijijini Ngarawani juzi, alisema wameshindwa kutangaza siku hiyo, badala yake wanajielekeza kwenye maandalizi ya tohara za watoto wa kiume ili kuepuka kuangukia mkono wa Serikali.
Marwa alisema suala la ukeketaji linahusu mila na desturi, hivyo inahitajika elimu kwa jamii hususan wanawake ambao wanakaa na watoto wa kike kubadili mitazamo. Aliomba elimu zaidi kutolewa badala ya sheria, ambayo matokeo yake hayajazaa matunda licha ya jitihada ambazo zimekuwa zikifanywa na Serikali.
Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu alisema Serikali imejipanga kuwadhibiti watu watakaojihusisha na ukeketaji kwa sababu athari zake ni kubwa kwa afya, kisaikolojia na elimu baada ya watoto wengi kuacha masomo na kuolewa.
Kupitia Mradi wa Tokomeza Ukeketaji Serengeti unaotekelezwa na Shrika la Amref na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa hisani ya Kitengo cha Umoja wa Mataifa cha kupinga ukatili wa kijinsia, makundi mbalimbali tayari yameelimishwa kuhusu madhara.
Mkuu wa Polisi wa Wilaya hiyo, Mathew Mgema alisema wenyeviti wa vitongoji na vijiji watakaohusika kuficha taarifa za ukatili huo katika maeneo yao watakamatwa.
Next
« Prev Post
« Prev Post
Previous
Next Post »
Next Post »
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
EmoticonEmoticon