KAMPUNI YA SIMON GROUP KUFISILIWA!!!

05:17

Dar es Salaam. Kampuni ya Simon Group Ltd inayomiliki kiwanda cha kukamua mafuta ya mbegu za pamba cha Nyanza Cotton Mill imewekwa chini ya uangalizi na kampuni ya Uwakili ya NexLaw, hali inayoashiria kuanza kufilisiwa.
Hatua hiyo imefikiwa takriban miezi miwili tangu Rais John Magufuli aiagize Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Mwanza kuhakikisha watu waliopora mali za Chama cha Ushirika cha Nyanza (NCU), wanapatikana na kuzirudisha mara moja.
Rais Magufuli alimtaja Mkurugenzi Mtendaji wa Simon Group, Robert Kisena ambaye pia ni mmiliki wa kampuni za Usafiri Dar es Salaam (Uda) na mwenye hisa nyingi kwenye mradi wa mabasi ya mwendo kasi (Udart) kuwa mhusika mkuu. Alisema Kisena alipewa Kiwanda cha New Era kwa Sh1 bilioni, lakini fedha aliyolipa ni Sh34 milioni tu.
“RC (Mkuu wa Mkoa) umezungumza kwamba katika miaka yote aliyepewa alikuwa anunue kwa zaidi ya bilioni moja, lakini amelipa milioni 34 tu na nasikia ni Simon Group,” alisema Magufuli.
Taarifa iliyotolewa jana na NexLaw ilisema majukumu ya wakurugenzi wa Simon Group yamesitishwa na mwenye mamlaka ya kupokea fedha zozote kutokana na mapato ya kampuni au kufanyia kazi ni muungano wa mawakili wa kampuni hiyo.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »