MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu soka Tanzania bara, Yanga leo watamenyana na Azam FC katika mchezo wa ligi utakaochezwa kwenye uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.
Timu zote mbili msimu huu hazijaanza vizuri lakini Azam ndio yenye hali mbaya zaidi baada ya kuendelea kuporomoka siku hadi siku. Kutokana na matokeo mabaya huenda timu hiyo leo ukamaliza hasira zake kwa Yanga ingawa hata Yanga haitakubali kupoteza mechi hiyo ikielekea kutetea taji lake.
Azam imefungwa na Ndanda FC mabao 2-1, ikatoka sare dhidi ya Ruvu Shooting mabao 2-2 na kufungwa na Stand United bao 1-0.
Kwa sasa timu hiyo kabla ya michezo ya jana ilikuwa inashika nafasi ya nane ikiwa na pointi 11 katika michezo saba iliyocheza.
Pia, Yanga baada ya kufungwa na Stand United bao 1-0, tayari ililipiza kisasi kwa Mtibwa Sugar katika mchezo uliopita kwa kuifunga mabao 3-1 kwenye uwanja wa Uhuru.
Timu zote mbili zitakuwa uwanjani zikiwa na kumbukumbu ya kukutana katika mechi ya ngao ya hisani iliyochezwa Agosti mwaka huu ambapo Azam iliibuka na ushindi kwa mikwaju ya penalti 4-1 baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 katika dakika za kawaida.
Yanga kabla ya michezo ya jana ilikuwa ikishika nafasi ya nne kwa pointi 14 katika michezo saba iliyocheza, ikiwa na kiporo kimoja.
Timu hizo kila zinapokutana hucheza kwa presha kila mmoja akitaka kupata matokeo mazuri.
Mambo hayatakuwa shwari iwapo kuna atakayekubali kipigo huenda, kocha mmojawapo kati ya Hans van Pluijm wa Yanga au Zeben Hernandez wa Azam akazidi kunyooshewa vidole na kuwa hatarini kutimuliwa.
Mchezo mwingine utakaochezwa leo ni Ruvu Shooting dhidi ya Mbeya City kwenye uwanja wa Mabatini Mlandizi.
Ruvu inashika nafasi ya 11 kwa pointi tisa katika michezo saba iliyocheza, huku Mbeya City ikishika nafasi ya saba kwa pointi 12 katika michezo tisa iliyocheza.
Mchezo huo huenda ukawa mgumu, kwani timu zote zinafahamiana na kila mmoja atahitaji kupata matokeo mazuri na kujiweka sehemu salama.
Next
« Prev Post
« Prev Post
Previous
Next Post »
Next Post »
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
EmoticonEmoticon