HII ni wiki ambayo shule nyingi za msingi na sekondari hapa nchini zimefunguliwa tayari kwa mwaka mpya wa masomo. Kwa wazazi wengi, hii ni wiki yenye changamoto za kipekee.
Tanzania ni taifa kijana kwa sababu zaidi ya nusu ya wananchi wake wana umri wa chini ya miaka 30. Hii maana yake ni kwamba watu wake wengi wanasoma ama shule ya msingi, sekondari au vyuoni.
Hata hivyo, ni jambo linaloumiza kwamba vijana wetu hawa –kwa ujumla wao, hawapati elimu ya darasani inayoweza kuwafanya wakawa washindani wa kweli katika dunia ya sasa.
Kwa takribani miaka 30 sasa, elimu yetu imekuwa ikiendeshwa shaghalabaghala. Kusema kweli, huwezi kuona ni wapi ambako tunataka kulipeleka taifa letu kielimu.
Hali hii ni tofauti na kipindi cha miaka 20 ya kwanza baada ya Uhuru wetu. Nchi yetu ilikuwa ikisifika kwa aina ya wasomi iliyokuwa ikizalisha karibu katika kada zote za kielimu.
Wapo viongozi wengi wa juu katika baadhi ya nchi za jirani ambao hadi leo wanashukuru kwamba walikuja Tanzania na kupata elimu bora iliyokuwa ikikaribiana, na wakati mwingine kulingana kabisa, na ile ya kwenye nchi zilizoendelea.
Ni lazima tukubaliane kwamba kutoka hapa tulipo kielimu tunahitaji maono na bungua bongo nzito. Ni lazima tuwe na maono yetu kama taifa ambayo yanashabihiana na ulimwengu tunamoishi.
Matamko pekee na jitihada za aina ya zimamoto haziwezi kututoa hapa tulipo. Mkwamo huu tutatoka tu endapo tutaamua kukaa pamoja kama taifa; pasipo kujali tofauti zetu zote na kuachia wataalamu watuelekeze na kutuwekea dira.
Mustakabali wa taifa hili utategemea zaidi aina ya elimu inayotolewa kwa vizazi vyake vya sasa na vijavyo. Kama tutakuwa na mfumo wa elimu wa hovyo, tusitegemee kuwa na mustakabali mwema.
Wajibu mkubwa, pengine kuliko wowote mwingine, wa kizazi chetu hiki ni kuhakikisha kuwa tunaweka msingi imara wa elimu kwa vizazi vyetu vijavyo.
Kwa kufanya hivyo, hata bila ya kuwa na dhahabu, gesi, mbuga za wanyama na utajiri mwingine wa rasilimali, Tanzania itabaki kuwa taifa la watu wa maana. Tofauti na hapo, vizazi vijavyo watatukana makaburi yetu.
Next
« Prev Post
« Prev Post
Previous
Next Post »
Next Post »
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
EmoticonEmoticon