MWENYEKITI mpya wa Azam FC, Idrissa Nassor ameweka wazi mikakati yake akisema kuwa atashirikiana na wenzake ili kuirejesha timu yao katika kiwango chake.
Nassor, ambaye alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Azam, juzi alithibitishwa kuchukua nafasi ya Mwenyekiti iliyoachwa wazi na Alhaji Said Mohamed baada ya kufariki dunia.
Aliliambia gazeti hili jana kuwa ni wakati wa kujipanga na kuirudisha timu kwenye kiwango kwasababu imeonekana kuyumba tangu kuanza kwa msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania bara.
“Baada ya kupewa jukumu jipya ni wakati wa kujipanga katika kuhakikisha timu yetu inafanya vizuri kwenye mzunguko wa pili wa ligi, ikiwezekana tuchukue ubingwa au kumaliza katika nafasi za juu,”alisema.
Nassor alisema bado wana imani kubwa wanaweza kuchukua ubingwa iwapo watafanya vizuri katika mechi za mzunguko wa pili. Alikiri kuwa kuna changamoto nyingi katika kufikia mafanikio wanayohitaji lakini ni lazima wapambane kukabiliana nazo.
Tayari Azam FC ilifanya usajili wa wachezaji wa kigeni kutoka Ghana Yahaya Mohamed na Samwel Afful kwa ajili ya kuongeza nguvu kwenye kikosi hicho kilichoonyesha kuyumba.
Azam FC inayoshika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi kwa pointi 25 nyuma ya Yanga yenye pointi 33 na kinara Simba 35. Inatarajiwa kuingia kambini Jumatatu ijayo, kwa maandalizi ya michuano ya mzunguko wa pili utakaoanza kutimua vumbi kuanzia Desemba 17, mwaka huu.
Next
« Prev Post
« Prev Post
Previous
Next Post »
Next Post »
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
EmoticonEmoticon