SERIKALI YARUHUSU MKUTANO WA SIMBA

07:39

SERIKALI imesema kuwa haizuii mikutano ya klabu za Simba na Yanga ila haipo tayari kuona bodi ya wadhamini inageuka kuwa wamachinga na kukodisha timu.
Akizungumza jana, Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa, Mohamed Kiganja alirusha dongo kwa Baraza la Wadhamini wa Yanga kwa madai kuwa limeshindwa kusimamia na kulinda mali za klabu hiyo.
“Kazi ya Baraza la Wadhamini ni kulinda mali za klabu, lakini baraza linageuka kuwa wamachinga na kukodisha klabu hiyo ndio hatutaki,” alisema Kiganja na kuongeza: "Katika uendeshaji wa soka tunatambua suala la uwekezaji, lakini ni lazima uzingatie kanuni na taratibu zilizowekwa. “Hatupingi klabu zetu kufanya mabadiliko isipokuwa tunajaribu kuwakumbusha kufuata utaratibu wa kisheria na katiba zao. Kwa sababu unapobadilisha jina au kufanya marekebisho yoyote, ni lazima vikasajiliwe na kutambulika,” alisema.
Kauli hiyo ya Kiganja ni dongo kwa Bodi ya Udhamini wa Yanga ambayo tayari imeingia mkataba wa kumkodisha Mwenyekiti wa klabu hiyo Yusuf Manji kwa miaka 10 akichukua asilimia 75 ya mapato huku klabu ikiambulia asilimia 25. Manji aliomba ridhaa hiyo ya wanachama ya kumkodisha timu kwa kile alichodai kuwa timu hiyo imekuwa ikijiendesha kwa hasara.
Akizungumzia mkutano mkuu wa dharura wa Simba uliopangwa kufanyika Desemba 11 kwenye Bwalo la Maofisa wa Polisi alisema “Sisi hatukatai mikusanyiko, wao wakutane walumbane lakini mwisho wa siku taratibu zifuatwe, nitamtuma Msajili kuhakikisha wanachama wote wanapata haki sawa ya kuuliza maswali kuepuka mapandikizi ambayo yamewekwa na viongozi.
“Kuna mkutano mmoja, mwanachama pandikizi anamwambia mwenyekiti funga mkutano, na mwenyekiti akafunga kweli, hiyo si sawa na klabu hizi za Simba na Yanga ndio zina desturi hii ya kuwaandaa watu wa kuzungumza hii si sawa, kila mtu apewe nafasi kwa uhuru.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »