Kuonyesha timu zina uchu wa ubingwa unaoshikiliwa na Yanga, baadhi yake zimeshaingia kambini kuanza maandalizi huku nyingine zikitarajiwa kuingia kambini wiki ijayo.
Timu zilizoingia kambini mapema wiki iliyopita ni Mtibwa Sugar, Mbao FC, Ruvu Shooting, JKT Ruvu na Kagera Sugar.
Bingwa mtetezi wa ligi hiyo, Yanga itaanza kambi yake ya maandalizi kesho chini ya kocha mkuu mpya, George Lwandamina ambaye juzi alitambulishwa rasmi baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili.
Lwandamina anarithi mikoba ya Hans Pluijm ambaye amepandishwa cheo na kuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa Yanga.
Meneja wa klabu hiyo, Hafidh Saleh aliliambia gazeti hili kuwa kikosi cha timu hiyo kitaanza kujifua kesho chini ya Lwandamina. Yanga itaanza na JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
“Taratibu zote zimekamilika na timu itaanza maandalizi Jumatatu (kesho) pale Viwanja vya Chuo cha Polisi Kurasini,” alisema na kuongeza kuwa kama watahamishia kambi nje ya nchi taarifa zitatolewa.
Vinara wa Ligi Kuu, Simba watakaoanza kwa kuifuata Ndanda FC Mtwara, wamepanga kuanza kambi wiki ijayo chini ya makocha Joseph Omog anayesaidiwa na Jackson Mayanja.
Omog na Mayanja wana kazi ya kurudisha ari na morari ya wachezaji baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo za kufungia mzunguko wa kwanza.
Katibu Mkuu wa Simba, Patrick Kahemele alisema jana kuwa kikosi kitaanza maandalizi wiki ijayo huku kamati ya usajili ikiendelea kusaka wachezaji kulingana na nafasi zilizopendekezwa na kocha Omog.
“Timu itaingia kambini wiki ijayo, lakini suala la usajili kamati husika inaendelea na mchakato, kambi itaanza na wachezaji waliopo, watakaoitwa wataungana na wenzao.”
Matajiri wa Azam wataanza kambi Desemba 2 huku kocha mkuu, Zebenzui Hernandez akisema atakuwa na kazi ya kurekebisha kasoro zilizojitokeza raundi ya kwanza sanjari na kuwaingiza kwenye mfumo wachezaji wapya waliosajiliwa hivi karibuni Yahya Mohamed na Samuel Afful.
“Tuna kazi kubwa ya kuhakikisha tunafanya maandalizi mazuri. Tumedhamiria kufanya vyema hivyo hatutaki yaliyotokea raundi ya kwanza yajirudie. Muda unakimbia na tumesajili wachezaji wapya ambao tunatakiwa kuwaingiza kwenye mfumo,” alisema Mhispania huyo.
Kocha msaidizi wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila alisema kikosi chao tayari kimeanza maandalizi na kuongeza kuwa kocha anatarajia kusajili wachezaji kutoka timu ya vijana. Mtibwa itakuwa ugenini kuanza na Ruvu Shooting.
“Sisi tumeshaanza maandalizi huku Manungu,tunaamini mzunguko wa pili utakuwa na mgumu na ndiyo maana tumeanza matayarisho mapema,” alisema.
Ofisa Habari wa Mbeya City iliyo katika hatari ya kumpoteza Joseph Mahundi anayetimkia Azam, Dismass Ten alisema mazoezi ya timu hiyo yataanza Novemba 30 baada ya kuwasili kwa kocha mkuu, Kinnah Phiri aliyekwenda mapumzikoni Malawi.
“Tunaendelea na utaratibu mwingine wa kiuongozi, timu itaanza kambi Novemba 30,” alisema Ten ambaye timu yake itaikaribisha Kagera Sugar.
Kocha mkuu wa Ruvu Shooting, Malale Hamsini alisema licha ya kuanza maandalizi mapema ya mzunguko wa pili, hatarajii kusajili mchezaji mpya kwa kuwa ana imani na kikosi chake.
“Ninatambua ligi ni ngumu lakini ninaamini kikosi changu kipo imara... sitarajii kusajili mchezaji mwingine bali natumia kipindi hiki kurekebisha na kuongeza ufanisi kwa wachezaji,” alisema.
Ofisa Habari wa Majimaji ya Songea, Athanas Charles alisema kuwa baada ya kuona walianza ligi vibaya na kumaliza mzunguko wa kwanza wakiwa wa 13, wameamua kuanza kambi mapema jijini Dar es Salaam kabla ya mzunguko wa pili kuanza.
“Ili kuhakikisha mambo hayo yote yanakwenda sawa ndiyo tumekubaliana viongozi na wachezaji kuanza kambi hapa Dar es Salaam na si Songea kama ilivyozoeleka ili ligi itakapoanza tuwe na kitu cha tofauti,” alisema
Kocha wa Mbao FC, Etiemi Ndayiragije, alisema wataingia kambini kesho (Jumatatu) kujiandaa na raundi ya pili.
Timu hiyo itakuwa mwenyeji wa ‘ Mwanza derby’ dhidi ya Toto Africans. “Ninaamini tukianza maandalizi mapema, tutafanya vizuri mzunguko wa pili… unajua maandalizi ya mapema yana faida nyingi, nimewaeleza vizuri wachezaji wangu namna ya kupata matokeo mazuri,” alisema Ndayiragije.
Alisema mzunguko wa pili wa ligi hiyo utakuwa mgumu kutokana na kila timu kuhitaji kupata ushindi ili kuweza kuchukua ubingwa, lakini timu nyingine zikiepuka kushuka daraja.
Mpaka sasa, timu za African Lyon ya Dar es Salaam, Toto African (Mwanza) na Prisons ya Mbeya hazijaweka bayana ratiba zao za kuanza kambi kujiandaa na mzunguko wa pili wa ligi hiyo.
Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, mzunguko huo utaanza Desemba 17 na unatarajia kukamilika Mei mwakani.
Mpaka sasa mshambuliaji wa Simba Shiza Kichuya ndiye anayeongoza kwa kupachika mabao tisa akifuatiwa na Amiss Tambwe wa Yanga mwenye mabao saba.

EmoticonEmoticon