KWANINI NCHI ZA AFRIKA KUACHANA NA ICC

06:07

Ilianza Burundi ikafuata Afrika Kusini na sasa ni Gambia. Orodha ya nchi zinazokusudia kujitoa kutoka Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) iliyopo The Hague, Uholanzi inazidi kuwa ndefu na wala haionyeshi kufikia mwisho.
Mtu atajiuliza, kwa nini nchi hizo zinaikimbia Mahakama iliyopewa jukumu la kuhukumu kesi zinazohusu uhalifu wa kivita, mauaji ya halaiki na uhalifu dhidi ya ubinadamu?
Hisia iliyoenea hasa barani Afrika ni kwamba Mahakama hiyo inatumia vipimo viwili tofauti katika kuwashtaki watu wanaotuhumiwa, hivyo ni ya kibaguzi.
Mfano mwananchi wa Burundi aliandika katika mtandao wa Twitter: “Umoja wa Ulaya na Marekani wanaua watu huko Pakistan, Yemen, Iraq, Syria, Palestina na Libya, lakini Mahakama ya The Hague inaiweka mbele Afrika katika kuamua watu wa kuwashtaki.” Alichapisha picha za watu waliofikishwa mbele ya Mahakama hiyo ambao wote ni Waafrika.
Gambia imetangaza kwamba “Mahakama hiyo ni ya Wazungu iliyoundwa kuwaandama na kuwadhalilisha watu wasiokuwa Wazungu.”
Gambia ni mojawapo ya nchi zenye tawala kandamizi kabisa katika Afrika, licha ya Rais wa nchi hiyo, Yahya Jammeh kuwa na ujasiri wa kusimama majukwaani na kujifanya kuwa msemaji na mtetezi wa Afrika. Mtawala huyo ana dukuduku.
Hajaisamehe Mahakama ya The Hague kwa vile ilikataa ombi lake la kutaka Umoja wa Ulaya ushtakiwe kutokana na kuuawa wakimbizi wa Kiafrika wanaokimbilia barani humo.
Serikali ya Gambia ilisema: “Nchi nyingi za Magharibi siyo chini ya 30 zimefanya uhalifu wa kutisha dhidi ya nchi huru za Afrika na raia wake na hakuna hata mhalifu mmoja wa kivita wa nchi ya Magharibi aliyeshtakiwa.”
Kiongozi Mkuu wa Mashtaka wa Mahakama hiyo ni Fatou Bensouda anayetoka Gambia. Pia, Rais wa Mkusanyiko wa Nchi Zilizotia Saini Mkataba wa Roma (ulioasisi ICC) ni Waziri wa Sheria wa Senegal, Sidiki Kaba.
Waziri huyo ameilaumu vikali hatua ya nchi za Kiafrika kujitoa kutoka ICC akisema Mahakama hiyo inahitaji iimarishwe na siyo kudhoofishwa.
Mwanzoni watawala kadhaa wa Kiafrika wa;oonyesha walifikiri kwamba mikono ya Mahakama hiyo itawafikia wapinzani wa Serikali zao au watu wanaojifanya ni wababe wa kivita na kwamba haitawagusa wao.
Hata hivyo, pale ilipoanza kuheshimiwa na watu wengi duniani ndipo ilipozidi pia kuwa kitisho hata kwa watawala wakorofi waliopo madarakani na pia pale watakapokuwa nje ya madaraka siku za usoni. Jambo hilo ndilo watawala wanahofia na wanataka kulizuia.
Kusakwa kwa al-Bashir
Mwaka 2009 Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitoa amri ya kukamatwa popote atakapopatikana Rais wa Sudan, Omar al-Bashir. Mahakama ya ICC baada ya kufanya upelelezi ilimshtaki rais huyo kwa kuendesha mauaji ya kimbari katika Jimbo la Darfur, magharibi ya nchi yake.
Tangu wakati huo al-Bashir amegeuka kuwa shujaa miongoni mwa watawala wa Kiafrika wasioitaka ICC. Amekuwa alama ya upinzani dhidi ya sheria za Kimagharibi ambazo viongozi kadhaa wa Kiafrika wanazitaja kuwa ni za kiimla.
Katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika (AU) mjini Kigali, Rwanda, Julai mwaka huu na pia huko Ethiopia, Sudan Kusini na Somalia ambako kote kuna kazi kubwa ya kufanywa na ICC, al-Bashir amepongezwa kuwa ni ‘kiboko’ mbele ya mataifa ya Magharibi.
Kenya, ikiungwa mkono na Chad ambayo ni mwenyekiti wa sasa wa AU ilipendekeza kwamba nchi zote za Afrika kwa pamoja zijitoe kutoka ICC.
Pendekezo hilo liligonga mwamba kutokana na ile kanuni kwamba kwa vile nchi za AU hazijaingia ndani ya mkataba wa ICC kama kundi moja, kwa hiyo haziwezi kujitoa kwa pamoja. Inatakiwa kila nchi ijitoe yenyewe - moja moja. Mkakati huo ndiyo unaotekelezwa sasa.
Nchi nyingi zaidi kujitoa?
Kuna ripoti zinasosema kwamba Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (nchi ambayo wababe wake kadhaa wa kivita wamefikishwa mbele ya ICC ) anafikiria kuitoa nchi hiyo kutoka ICC. Bunge la Kenya mara mbili lilipiga kura nchi hiyo ijitoe kutoka Mahakama hiyo, ikikumbukwa kwamba Rais wa nchi hiyo, Uhuru Kenyatta na Makamu wake, William Ruto waliwahi kufika huko The Hague kujitetea kutokana na mashtaka yaliyowakabili.
Serikali ya Uganda ambayo iliiomba Mahakama hiyo iwaandame na iwapeleleze na kuwashtaki viongozi wakuu wa waasi wa Lord Resistance Army (LRA), ilitangaza Oktoba kwamba inafikiria kuchukua hatua ya kujitoa kutoka ICC.
Sababu? Kuna tetesi kwamba ICC ilitaka kufanya uchunguzi juu ya uhalifu uliofanywa na wanajeshi wa Uganda kaskazini mwa nchi hiyo walipokuwa wanapambana na LRA.
Pia, Waafrika wanataka majaji wa Kiafrika wawahukumu watuhumiwa wa Kiafrika na kesi zao zifanyike Afrika. Jaribio kama hilo lilifanywa mwaka huu kwa kesi ya aliyekuwa Rais wa Chad, Hissene Habre.
Yeye alishtakiwa Dakar, Senegal, mbele ya Mahakama Maalumu ya AU kujibu mashtaka yakiwamo ya uhalifu dhidi ya ubinadamu, uhalifu wa kivita, kutesa watu na hata kushiriki katika ubakaji.
Habre alipatikana na hatia na akapewa kifungo cha maisha gerezani. Tukio hilo lilidhihirisha kwamba mtawala mkorofi aliyekwenda kinyume na haki za binadamu anaweza kutiwa pingu na kutupwa jela katika ardhi ya Kiafrika. Huo ulikuwa ushindi wa haki.
Mahakama kwa Afrika nzima ili kuwashtaki waliofanya vitendo vya uhalifu sawa na vile vilivyoorodheshwa na Mahakama ya ICC, siyo rahisi kuipata. Vikwazo mbalimbali vinatajwa kufikia jambo hilo na Mahakama kama hiyo kufanya kazi kwa haki na uhuru.
Hiyo inatokana na mazingira ya kisiasa yaliyoko katika nchi kadhaa za Afrika ambayo yanabinya uhuru na mara nyingi wanaoshikilia madaraka kutoujali utawala wa sheria.
Mkasa wa Habre ulikuwa ni tukio la kipekee, tena na la vuta nikuvute iliyozunguka kesi hiyo, mshtakiwa mwenyewe na wadau wengine wa ‘sarakasi’ hiyo.
Ilichukua miaka 25 tangu alipinduliwa kutoka madarakani huko N’djamena hadi alipohukumiwa mjini Dakar. Alikingiwa kifua na marais kadhaa wa nchi za Kiafrika waliopinga kufikishwa kwake mahakamani akiwamo Rais Abdoulaye Wade wa Senegal, nchi ambayo ilimpa hifadhi ya ukimbizi.
Kutokana na kuminywa na Umoja wa Mataifa na baada ya Wade kuondoka madarakani ndipo ilipopatikana njia ya kumshtaki Habre. Ili kujiepusha na kashfa ya kutuhumiwa kwamba inamlinda Habre, mtu ambaye anatuhumiwa kwa uhalifu mkubwa wa kuendesha mauaji ya kimbari, ndipo AU ilipoafikiana na Senegal kwamba ashtakiwe Dakar. Itaendelea wiki ijayo.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »