ZANZIBAR KUNUNUA MELI MBILI MPYA

06:23

WIZARA ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji imeanza mchakato wa ununuzi wa meli mbili mpya, ya abiria na mizigo na nyingine ya mafuta ili kusaidia huduma zinazotolewa na Mv Mapinduzi II.

Hayo yalisema Ikulu jana mjini hapa na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Balozi Ali Abeid Karume aliyefuatana na uongozi wa wizara yake katika mazungumzo na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein.

Aliwasilisha taarifa ya Utekelezaji wa Mpango Kazi kwa kipindi cha Julai hadi Septemba katika Bajeti ya mwaka 2016/2017. Balozi Karume alisema hatua hiyo itaimarisha sekta ya usafirishaji huku akieleza hatua zinazochukuliwa katika kuimarisha miundombinu ya usafiri wa bahari ikiwemo minara na maboya ya kuongozea meli.

Alisema wizara imeendelea kusimamia huduma za usafiri wa baharini kwa kusimamia usalama wa watumiaji na kuandaa kanuni za kimataifa na kuandaa Mpango Mkakati wa Uokozi.

Akizungumzia uimarishaji wa miundombinu ya usafiri wa anga, waziri huyo alieleza juhudi zinazoendelea katika ukamilishaji wa ujenzi wa jengo jipya la abiria lililopo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amaan Karume.

Alisema wizara yake kupitia Shirika la Nyumba na Wakala wa Majengo inaandaa Mpango Mkakati wa kuimarisha sekta ya makazi ya umma kwa kuzifanyia marekebisho nyumba za maendeleo Unguja na Pemba zikiwemo za vijijini pamoja na ujenzi wa nyumba mpya za bei nafuu nje ya miji.

Katika kuimarisha sekta ya mawasiliano, wizara hiyo inaendelea kutayarisha mpango mkakati wa miaka mitano wa mawasiliano Zanzibar, pamoja na uandaaji wa Sheria ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kurahisisha utumiaji wa sera ambayo inaondoa kasoro zinazojitokeza katika matumizi ya miundombinu ya mawasiliano.

Pamoja na hayo, Waziri alielezea kusikitishwa kwake na baadhi ya wananchi wanaofanya uharibifu wa makusudi katika nyumba zilizomo katika Mamlaka ya Mji Mkongwe hasa pale wanapotakiwa kuhama ili kupisha ujenzi.

Naye Dk Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa uongozi na watendaji wa wizara hiyo kwa juhudi wanazozichukua katika kutekeleza majukumu yao sambamba na kuwatumikia wananchi katika kuwaletea maendeleo endelevu.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwahudumia wananchi kwa kuimarisha huduma za usafiri na usafirishaji, mawasiliano na ujenzi. Aidha, alipongeza ushirikiano mzuri uliopo ndani ya wizara hiyo huku akiusifu uwasilishaji wa Mpango Kazi wake.

Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd aliipongeza wizara hiyo kuitaka kuchukua juhudi za makusudi kupitia shirika lake la nyumba kuzitambua nyumba zote za serikali pamoja na kutambua wapi zilipo.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »