TAMU NA CHUNGU STAND UNITED

05:20

MIKIKIMIKIKI ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara inaendelea kushika kasi kwenye baadhi ya viwanja vya vya soka nchini na kushuhudia matukio mbalimbali yakiendelea kutokeza viwanjani humo.
Ligi hiyo ambayo kinara wake ni klabu ya Simba, imekuwa na matukio ya ajabu kwa mashabiki kuvunja viti, kuvunja mageti na masuala mengine ambayo si afya ya soka la Tanzania, ambalo wakati huu linajikongoja.
Licha ya hali ya mambo kuwa hivyo, lakini kumejitokeza suala la timu ya Stand United kuwa miongoni mwa timu tatu za juu katika msimamo wa Ligi Kuu, ikiwa juu ya timu maarufu kama Yanga, Azam na Mtibwa.
Timu hiyo inayoshika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo imekuwa katika matatizo ya kiuongozi na kufanya aliyekuwa mdhamini wao, kampuni ya Uchimbaji Madini ya Acacia kujiweka kando, kuogopa kuchafuliwa na mgogoro huo wa viongozi wa pande mbili.
Licha ya hali ya mambo kuwa hivyo klabuni hapo, haijawafanya wachezaji kusahau majukumu yao na kushindwa kucheza na wao kuwa sehemu ya mgogoro. Kinyume chake, wachezaji hao wameweza kuungana vyema na kufanya vizuri uwanjani na kuifanya timu ishike nafasi hiyo mpaka wakati huu ambao ligi imefikisha michezo 10 kwa baadhi ya timu.
Baada ya Raia Mwema kuona mfululizo wa matokeo mazuri kikosini humo licha ya kuwepo matatizo ya kiuongozi, iliwatafuta baadhi wa wachezaji kuzungumza nao jinsi timu hiyo inavyoendeshwa licha ya hali ya mambo kuwa hivyo kikosini.
Nahodha Jacob Massawe alisema licha ya timu yao kuwa katika mgogoro wa kiuongozi hiyo wao haiwahusu na wanachokifanya ni kutimiza majukumu yao kama wachezaji.
Alisema mpaka kufika waliko sasa ni juhudi binafsi za aliyekuwa mwalimu wao raia wa Ufaransa, Patrick Jean Ulysses Liewig, ambaye sasa amerejea kwao. Massawe alisema mwalimu huyo ndio siri ya wao kufanya vizuri mpaka kufikia hivi sasa.
“Liewig ni kati ya walimu bora niliowahi kufanya nao kazi katika maisha yangu ya mpira wa miguu. Huyu anamfanya kila mchezaji awe rafiki yake na mtu ambaye hawezi kwenda sawa na mwalimu huyu ni lazima amuone mwalimu wa tofauti, lakini jamaa bonge la mwalimu.
“Muda wote anapenda wachezaji mshike kile anachokitoa kwenye mazoezi na kila akija mazoezini huja na kitu kipya tofauti na baadhi ya walimu wengine hurudia mazoezi kwa kukosa ubunifu katika uwanja wa mazoezi.
“Kama mchezaji ukiwa muelewa na kichwa chepesi ni rahisi kumuelewa Liewig, lakini ukiwa hauko makini unaweza kumchukia na kuona sio kocha mzuri kumbe hapana” alisema Massawe.
Massawe alisema faida nyingine ya mwalimu huyo ni kila mechi huja na mpango mwingine tofauti na mpango wa mechi iliyopita na wakati mwingine hubadili hata wachezaji kikosini kutokana na wapinzani jinsi walivyo.
Alisema hata yeye mwenyewe amezoea kucheza nafasi ya kiungo wa pembeni, lakini Liewig amemrudisha nafasi ya kiungo wa kati na kucheza vyema. “Mwalimu huyu hategemei wachezaji 11 na hutumia au hubadili mazoezi kutokana na aina ya mchezo tunaokwenda kukutana nao.
“Kabla ya michezo yetu huwasoma wapinzani jinsi wanavyocheza na akija katika uwanja wa mazoezi hutuletea kile alichokiona kwa wapinzani na kusema mchezo huu twende kwa mtindo gani na tutatumia wachezaji wa aina gani, kiukweli huyu ni bonge la kocha” alisema Maasawe.
Nahodha huyo aliendelea kusema kuwa moja ya vitu anavovishangaa kwa mwalimu huyo ni kila inapofika siku ya mchezo hapendi kuzungumza mara kwa mara na mara nyingi huwataka wachezaji wake kufika uwanjani mapema kwa ajili ya kutoa maelekezo ya mwishoni kabla ya mchezo wenyewe.
“Walimu wengi siku ya mchezo huwa na vikao vingi na kupeana maelekezo ya kila wakati, lakini kwa Liewig maisha hayako hivi yeye siku ya mchezo ndio kwanza hujitenga na mara nyingi hupenda kukaa mwenyewe na kumtaka kila mchezaji aweke akili yake katika mchezo husika.
“Isipokuwa yeye huwa anapenda tuwahi kufika uwanjani atoe maelekezo ya mwishoni kabla ya mchezo wenyewe” aliendelea kusema.
Massawe alifichua kuwa mazoezi ya mwalimu huyo ni mazuri kwa mchezaji anayekwenda kucheza soka la kulipwa barani Ulaya kutokana na sehemu nyingi za majaribio ya huko hutoa mazoezi kama ya mwalimu huyo.
Katika mojawapo ya mazungumzo aliyowahi kufanya na kocha wake, Massawe anasema Liewig aliwahi kumwambia kuwa mazoezi anayowapa ndiyo ambayo hutolewa na makocha wa barani Ulaya na kuwa mchezaji atakayeweza kuyavumilia, hatapata shida akienda kucheza soka la kulipwa.
Mchezaji mwingine wa timu hiyo, Kelvin Sabato Kongwa ‘Kev Kiduku’, alisema hali ya umoja kama timu ndio inayoleta matunda hayo kikosini mwao. Kongwa alisema kutokuwa na makundi kwa wachezaji ndiko kunakoleta matunda hayo.
“Kuna baadhi ya timu huwa zinafanya vizuri lakini hakuna umoja na mshikamano sasa timu kama hiyo ni rahisi kushuka chini. Sisi mpaka unaona tuko hivi wenyewe tunaishi vyema ambaye hachezi katika kikosi cha kwanza hamnunii mchezaji anayecheza, hivyo unavyokuwa na timu yenye umoja kama hiyo kuna kitu kizuri lazima mkifanye” alisema Kongwa.
Kongwa alisema masuala ya uongozi hawezi kuyazungumzia, lakini anashukuru kuona timu yao iko katika hali nzuri licha ya kuwa na matatizo.
Hata hivyo Raia Mwema liliwafatafuta baadhi ya viongozi wa zamani na wa sasa wa timu hiyo ili kuzungumza nao hali ya mambo ndani ya Stand United na kufanikiwa kuzungumza na mmoja wa viongozi wa zamani aliyekataa kutajwa jina lake gazetini na kusema timu hiyo ina hali mbaya na wachezaji hawajalipwa mishahara yao kwa miezi mitatu sasa.
Mmoja ya viongozi hao alisema wanachokifanya wachezaji wa timu hiyo kupambana uwanjani ni kitu kizuri lakini kwa hali ya mambo ilivyo sasa timu hiyo itaanza kuporomoka.
“Timu ina hali mbaya sana ndio maana hata kocha Liewig ameondoka na ametuma barua pepe kwa baadhi ya viongozi wa zamani na wa sasa, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, akionyesha kukerwa na baadhi ya mambo katika timu.
“Lakini shida kuu ilikuja ndani ya timu ile pale tu Acacia walipokuja kuweka fedha. Nafahamu kuna viongozi walikuja kuchota fedha na kwenda kufanya mambo yao, ukitaka kuamini hili mpaka sasa hakuna kiongozi anayejifanya yu karibu na timu, Raia Mwema limeambiwa.
Katika barua pepe ya Liewig, ameandika kila kitu ikiwamo kufichua kwamba kuna watu walimfuata kutaka auze mechi dhidi ya Mbeya City iliyofanyika Oktoba 7, katika uwanja wa Sokoine Mbeya, lakini alikataa hali hiyo na kuwaambia wachezaji wake licha ya ukata walionao lakini wasifanye mambo ya kuuza mechi.
Raia Mwema, liliutafuta uongozi wa sasa na kuzungumza na Ofisa Habari wa timu hiyo, Deokaji Makomba, na kiongozi huyo kusema kuondoka kwa Liewig hakujawashitua zaidi kumewashangaza kutokana na mwalimu hiyo kuondoka bila kuaga huku bado wakiwa na mkataba.
Alisema Liewig kaondoka na hajatuma barua pepe kwa kiongozi yeyote na taarifa zinazoendelea kuzagaa kwa watu wengine ni taarifa za uzushi.
“Mwalimu ameondoka na kila mmoja ameshangaa mazingira aliyoondokea, lakini si vibaya maana tangu ameondoka yeye tumekuwa tukiendelea kufanya vizuri.
“Tunakiri kuwa na ukata klabuni, lakini hali hii imetokana na mdhamini wetu kujitoa bila sababu za msingi, lakini tutalishughulikia suala hili limalizike na timu iendeleaa kufanya vyem kama ilivyoanza ligi,” alisema.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »