Dar es Salaam. Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Yusuf Manji haelezi undani wa nini kilisababisha deni la Sh 11.6 bilioni anazoidai anaidai klabu hiyo hadi sasa.
Uchambuzi wa gazeti hili na wadau wengine umebaini mambo 10 yaliyosababisha deni hilo ambalo katika mkutano wa dharura wa wanachama uliofanyika Agosti 6, Manji alisema lilitokana na matumizi makubwa ya uendeshaji.
Deni hilo limeacha maswali 10 ya wanachama, mashabiki wakihoji ukubwa wa fedha hizo, nani mdai ambaye hatajwi ingawa Manji amekuwa akisema klabu hiyo inadaiwa na yeye yuko tayari kulipa.
1- Aliingia Yanga kuifunga Simba
Manji aliyeingia madarakani 2012, alikuwa na mambo mawili makubwa. Mosi, ni kuifunga Simba iliyoinyanyasa Yanga kwa muda mrefu ikiwamo kipigo cha mabao 5-0. Kwa sababu hiyo, Manji alitumia fedha nyingi kuipa nguvu Yanga ili ilipe kisasi kwa Simba.
Pili, ni kuipa Yanga ubingwa, hivyo kutoa fedha nyingi za usajili uliofanikisha azma hiyo kwani tangu 2012, Simba haijaonja ubingwa.
2-Fedha za kuibomoa Simba
Ili kufanikisha azma yake ya kuharibu mafanikio ya watani, Simba, Manji alitoa fedha ili kumaliza utawala wa Simba kwa kuwachukua baadhi ya wachezaji.
Alianziaa kwa beki Kelvin Yondani, wakafuata kipa Juma Kaseja na Emmanuel Okwi, pia akiwaliza Simba kwa kumnasa beki wa APR, Mbuyu Twite, aliyeibukia Yanga baada ya Simba iliyotangulia Rwanda kumsajili. Msimu huu, alimsajili beki Hassan Ramadhan ‘Kessy’, ambaye bado ana mzozo na klabu yake ya zamani, Simba.
3-Kushindwa biashara ya jezi
Jezi ni jukumu lililochangia kuipa deni Yanga na kama Manji angeisimamia vizuri biashara hiyo na vifaa vingine, Yanga ingeingiza mapato mengi, isingekuwa na madeni. Hata hivyo, amewaachia wajanja watengeneze, kuuza vifaa mbalimbali vyenye nembo ya klabu hiyo na kujipatia fedha.
4-Usajili na mishahara
Hiyo ni sehemu ambayo Manji amechangia kuiingiza deni Yanga kwani amekuwa hana shida kwenye utoaji fedha za usajili ili kuwafurahisha mashabiki.
Jambo hilo lilisabababisha hasara baada ya wachezaji kutoka nje ya nchi waliotua Yanga kushindwa kuonyesha makali. Hao ni; Jama Mba, Genlison Santos ‘Jaja’, Emerson, Ernest Boakye na Isaack Boakye na wengineo.
5- Kubadili makocha
Tabia ya kubadili makocha mara nyingi imeigharimu Yanga kifedha ambayo imejikuta ikiingia kwenye deni. Manji amekuwa akiwaleta makocha wenye sifa kubwa, kuwalipa mishahara mikubwa, ingawa hawakudumu.
Baadhi yao; ni Kostadian Papic, Milutin Sredojevic ‘Micho’, Sam Timbe, Ernest Brandts, Tom Santifiet na sasa Hans Pluijm.
6-Kuvurunda kimataifa
Mashindano ya kimataifa yakiwamo Ligi ya Mabingwa Afrika, Kombe la Shirikisho yana fedha nyingi, lakini kama ni pale timu inapoingia hatua ya makundi.
Tangu Manji atue Yanga, imekuwa ikipishana na fedha hizo kwa kushindwa kuingia hatua ya makundi na kuishia hatua ya awali na kuzikosa fedha hizo.
Msimu huu, ilijitahidi kufika hatua ya maundi ya Kombe la Shirikisho na kushika nafasi ya nne kwenye kundi lao, hivyo kuambulia Dola 150,000, sawa na Sh300 milioni.
7- Kushindwa kuanzisha Yanga TV
Hilo ni jambo lingine lililochangia Yanga kukosa mapato na kujikuta ikikumbwa na deni. Manji alipoingia madarakani aliahidi kuanzisha televisheni, jambo ambalo hadi sasa ni ndoto ambayo ingeingiza mapato makubwa kutokana na matangazo.
Mgogoro na Azam TV kwenye mkataba wa kurusha matangazo ya Ligi Kuu ambao Manji alisusia fedha hizo kwa miaka mitatu, zingesaidia uendeshaji wa Yanga, hivyo kuepusha madeni.
8- Uwanja
Jambo linaolitesa Yanga na kuikosesha mapato ni uwanja ambao ungeingiza fedha kutoka kwa mashabiki, matangazo na hata kukodishwa kwa timu nyingine. Ahadi ya Manji ya kuijengea Yanga uwanja haijaitimizwa.
9-Ziara nje ya nchi
Ziara za nje ya nchi zilisababisha Yanga iingie gharama. Timu hiyo iliweka kambi mara mbili Uturuki ikiwa chini ya Manji.
10-Kuingia bure uwanjani
Manji amekuwa na utaratibu wa kuruhusu mashabiki kuingia bure uwanjani. Alifanya hivyo kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho, hatua ya makundi dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo.
Wasemavyo wadau
Kocha wa zamani wa Taifa Stars, Dk Mshindo Msola alisema deni kubwa Yanga na anayeidai vinatakiwa kuwekwa wazi.
“Kuna usiri unaofanya watu washindwe kuelewa. Manji anaweza kuwa na lengo zuri, lakini usiri wa deni unatia shaka kwani fedha hizo siyo ndogo. Huyo anayesemwa kuwa mdai lazima atoe uthibitisho. “Mfano, kambi za Uturuki a ilizokwenda Yanga, aligharimia yeye (Manji) au alishirikiana na viongozi? Je, alifanya hivyo kwa masilahi binafsi, halafu deni ipate klabu,” alihoji Msola.
EmoticonEmoticon