MWENYEKITI wa Yanga, Yusuf Manji amesema mkutano mkuu wa dharura unaotarajiwa kufanyika kesho utakuwa huru na wa haki na kila mwanachama hai atapewa nafasi ya kutoa duku duku lake kabla ya makubaliano kufikiwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Manji aliwataka wanachama wa klabu hiyo kujitokeza kwa wingi kwenye mkutano huo utakaofanyika makao makuu ya klabu hiyo Jangwani, Dar es Salaam kwa ajili ya kujadili masuala mbali mbali likiwemo lile la ukodishwaji wa klabu hiyo.
“Mkutano utakuwa huru na wa haki kwa kila mwanachama ambaye amelipia kadi yake atapewa nafasi ya kutoa maoni na dukuduku lake kabla ya makubaliano kufikiwa,” alisema Manji.
Pia Manji alisema amesikia kwenye vyombo vya habari (siyo gazeti hili) kuwa Katibu wa Baraza la Wazee la Yanga, Ibrahim Akilimali kuwa hajalipa ada ya uanachama, jambo ambalo linamwondolea sifa ya kuwa mwanachama, lakini Akilimali amelithibitishia gazeti hili kuwa yeye ni mwanachama hai kwani kadi yake amelipia mwaka mzima.
Hata hivyo, Akilimali akizungumza kwa simu na gazeti hili baadae jana, alisema kuwa yeye ni mwanachama halali na ana haki ya kuhudhuria mkutano huo kwani amelipia kadi yake kwa mwa mmoja. Alisema tangu alipie kadi yake ni miezi sita imepita hivyo bado ana miezi sita mingine kabla ya kumalizika muda aliolipia wa mwaka mmoja.
Manji alisema baada ya makubaliano hayo ya mkutano mkuu huo kufanyika uwanja wa mazoezi utaanza kujengwa ndani ya siku 90 katika eneo la Gezaulole lililopo Kigamboni kwa mujibu wa mkataba uliosainiwa na kampuni ya Yanga Yetu.
Aidha, Manji alisema kuhusu suala la kusainiwa kwa mkataba na bodi ya wadhamini dhidi ya kampuni ya Yanga Yetu kila kitu kitajadiliwa kwenye mkutano huo, ambapo wanachama wametakiwa kuwahi mapema huku ulinzi ukiwa wa uhakika.
Alisema kama kutakuwa na mgongano wa kimaslahi kati yake na Yanga, basi wanachama ndio watakaoamua kama anaweza kuendelea au kukaa kando, yuko tayari kutii uamuzi wowote.
Manji alisema badala ya wanachama kukimbilia kwenye vyombo vya habari kuzungumza kuhusu masuala ya klabu wanatakiwa kujitokeza kwa wingi kwenye mkutano huo ili kuchangia kwa manufaa ya Yanga.
Mkutano huu wa dharura unafanyika huku kukiwepo sintofahamu ya namna mkataba wa ukodishwaji wa klabu ya Yanga kwa kampuni ya Yanga Yetu ulivyosainiwa huku ukikiuka baadhi ya taratibu muhimu.
Next
« Prev Post
« Prev Post
Previous
Next Post »
Next Post »
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
EmoticonEmoticon